Muziki unaimarisha ubongo na uwezo wa kukumbuka – Wataalamu
NA BENSON MATHEKA
IKIWA husikilizi muziki, unakosa kitu muhimu kwa afya yako ya akili, kulingana na wataalamu.
Kusikiliza muziki ni njia moja ya kuimarisha uwezo wa akili yako sawa na mazoezi ya kila mara.
Wataalamu wa afya wanasema sio rahisi kwa watu wanaofanya mazoezi kila mara kusahau mambo kwa kuwa ubongo wao huwa imara.
Mazoezi pia hufanya ubongo kuwa thabiti mtu anapozidi kuzeeka. Wataalamu wanasema kuwa mazoezi na kusikiliza muziki ni miongoni mwa njia ambazo mtu anaweza kuboresha ubongo wake.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya ubongo, mazoezi hufanya mtu kudumisha uwezo wa kukumbuka mambo.
“Mazoezi sio tu kuimarisha viungo vya mwili bali pia huimarisha uwezo wa akili. Mazoezi ni muhimu kwa kuondoa mfadhaiko na matatizo ya akili. Utafiti unaonyesha kuwa mazoezi kiasi yanafanya mtu kuepuka mfadhaiko. Ni muhimu kufanya mazoezi kuimarisha afya ya akili,” asema mtaalamu wa afya ya ubongo Dkt Sarah Kalekye.
Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Havard ulionyesha kuwa kukimbia kwa dakika 15 kwa siku au kutembea kunapunguza uwezekano wa mtu kupata matatizo ya akili kwa asilimia 26.
Utafiti huo ulionyesha kuwa kudumisha mazoezi kila siku kunaepusha mtu kurejea katika hali ya mfadhaiko na huzuni.
“Mazoezi hupigana na huzuni na matatizo ya akili kwa sababu yanafanya mtu kuhisi vyema,” asema Dkt Kalekye.
Mazoezi pia hufanya mwili na ubongo kuwa na mawasiliano mazuri na pia huchangia seli zaidi kukua.
Wataalamu wanapendekeza watu kufanyia mazoezi nje ya nyumba kwa sababu kuna manufaa zaidi.
“Kama unafanyia mazoezi yako nje ya nyumba, basi inakuwa bora kwa sababu utakuwa na manufaa zaidi ya kupata vitamini D. Fanyia mazoezi katika mazingira mapya na njia mpya ili upate faida zaidi ya kukuza ubongo,” asema Dkt Kalekye.
Wanasaikatrikia pia wanasema njia nyingine ya kuboresha ubongo ni kusikiliza muziki.
Kulingana na Dkt Albert Tumaina, mwanasaikatrikia katika hospitali ya Ponya, Nairobi, muziki huwa unachangamsha ubongo.
“Kuna ushahidi kuwa muziki unaboresha ubongo kwa njia ya kipekee. Wakati mtu anaposikiliza au kucheza muziki ubongo wake wote huwa unashiriki. Jiunge na kikundi na waimbaji au lipa tikiti kuhudhuria tamasha za bendi unayoipenda kwa sababu kufanya hivi kunachangia kuimarisha ubongo wako,” asema Dkt Tumaina.
Ingawa watu wengi huwa wanaepuka kufanya kazi za sulubu shambani, wataalamu wanasema kwamba ni njia mojawapo ya kuimarisha ubongo.
“Kufanya kazi shambani ni muhimu kwa sababu kunafanya mtu kufikiria,” asema na kuongeza kuwa kujifunza kukariri vitu pia kumetambuliwa kama njia ya kujenga ubongo kuwa imara.
“Jifunze kukariri vitu. Hii ni mbinu ambayo pia inatumiwa na wacheza filamu. Kama unajaribu kukariri maneno fulani au kujaribu kujifunza kitu huku ukitembea tembea, unaweza kushika kwa njia rahisi kile unachokariri. Kwa njia hii unaimarisha ubongo wako,” asema Kalekye.
Anasema kwamba lishe bora ni muhimu kwa kukua kwa ubongo ikiwa halina sukari kwa wingi.
Karibu asilimia 20 ya sukari au chakula cha kutupa nguvu tunachokula kinaelekea kwa ubongo, na kuufanya ubongo kutegemea sana sukari.
Hivyo basi, wataalamu wanapendekeza watu kupunguza kiwango cha sukari kwa kuwa kinaathiri uwezo wa ubongo.
Ikiwa viwango vya sukari haviwezi kudhibitiwa, akili ya mtu itahisi kuchanganyikiwa.
Seli za ubongo hujengwa kwa mafuta, kwa hivyo ni muhimu kutotoa mafuta kutoka kwa chakula chako. Mafuta kutoka kwa njugu, nafaka, parachichi na samaki ni muhimu kwa afya ya ubongo. Kulingana na mtaalamu wa lishe James Karuku, mafuta yanafaa kuwa ya wastani kwa kuwa yanaweza kuathiri mwili.
Wataalamu wa masuala ya akili wanasema kwamba uchovu unaweza kudhoofisha uwezo wa akili. Wanashauri watu kupumzika vya kutosha ili kuweza kudumisha akili zao katika hali bora.
“Ni muhimu kupumzika. Msongo wa muda mrefu huathiri sana ubongo.
Kwa hivyo, ni muhimu kujua kuwa tunastahili kupumzika mara moja kwa wakati fulani kuwezesha pia ubongo kupumzika,” Tumaina
Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa wakati mwingine mawazo ni muhimu kwa sababu yanatuwezesha kuchukua hatua za haraka wakati wa dharura. Wanasema watu wasiotaka changamoto za maisha huwa wanadhoofisha uwezo wa akili zao.
“Ni muhimu kutafuta njia za kujipa changamoto.
Njia muhimu ya kuboresha ubongo wako ni kuupa changamoto kwa kujifunza kitu kipya kabisa. Kwa mfano kujifunza kuchora au kujifunza lugha mpya huchangia ubongo kuwa bora zaidi. Unaweza pia kucheza michezo ya mitandaoni dhidi ya marafiki au watu wa familia,” aeleza Tumaina.
Kupata usingizi wa kutosha, aeleza, Tumaina, pia kunachangia kufanya ubongo kuwa imara.
Unapolala, mawasiliano huwa dhabiti na huwa unakumbuka kile umejifunza wakati wa mchana.
Kwa hivyo kulala ni kitu muhimu katika kuimarisha kumbukumbu.