Muziki: Wito kizazi cha sasa Kenya kiige kina Nameless, Jua Cali
NA WANDERI KAMAU
KATIKA miaka ya 2000, Kenya ilisifika pakubwa kutokana na muziki wake wa kizazi kipya wakati huo, uliojulikana kama ‘Kapuka’.
Hiyo ndio ilikuwa sauti iliyoipa Kenya utambulisho maalum katika eneo la Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote.
Kabla ya Kenya kukumbatia sauti hiyo, Wakenya wengi walikuwa wamezamia kwenye miziki aina ya Lingala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Reggae kutoka mataifa kama Jamaica.
Hata hivyo, ujio wa wanamuziki kama Nameless, Wahu, Redsan, Titi Solomon, Mr Googz, Jua Cali, Vini Banton kati ya wengine wengi, ulianza kuinua bendera ya Kenya kimuziki Afrika Mashariki na barani Afrika.
Pia, kulikuwa na makundi mengine ya wanamuziki yaliyochipuka kuendeleza sauti mpya ya Kenya kimuziki kama vile Kleptomaniax, P-Unit, Tatuu, Camp Mullah kati ya mengine mengi.
Kikweli, Kenya ilivuma sana kimuziki, na kufanikiwa kuyapita mataifa jirani kama Tanzania na Uganda.
Wakati huo, baadhi ya wanamuziki waliovuma nchini Tanzania walikuwa Ali Kiba, Mr Nice, Dudu Baya, TID, Matonya kati ya wengine.
Mastaa waliochipuka baadaye kama Diamond Platnumz hawakuwa wakisikika.
Nchini Uganda, mwanamuziki Jose Chameleone, Bebe Cool na Juliana Kanayamozi ni miongoni mwa wale walioonekana kuwa ‘mabalozi’ wake wa kimuziki katika taifa hilo.
Kenya iliwika pakubwa, kwani wanamuziki wake walikuwa wakishinda tuzo kubwa kubwa na za kifahari za muziki kama vile Tuzo za Kisima, Tuzo za Kilmanjaro na Tuzo za KORA (zilizokuwa zikiandaliwa nchini Afrika Kusini).
Nyakati hizo, mwanamuziki yeyote aliyeshinda Tuzo za KORA alikuwa akiheshimika sana.
Baadhi ya wanamuziki kutoka Kenya waliowahi kushinda tuzo hizo za kifahari ni Nameless na Wahu.
Hata hivyo, baada ya Kenya kuwika kimuziki na kutikisa anga ya Afrika Mashariki kwa karibu miaka 20, hali imeanza kubadilika.
Wadadisi na wafuatiliaji wa masuala ya burudani wanasema kuwa Kenya “imeanza kujikwaa kimuziki” kwani kizazi kilichopo kinatunga miziki ambayo haikai kwa muda mrefu na haina utambuzi wa kimataifa.
Bw John ‘Mosh’ Muchiri, ambaye ni mwanahabari mkongwe wa masuala ya burudani ambaye shughuli zake nyingi ziko jijini London nchini Uingereza, anasema Kenya inafaa kutathmini mwelekeo wake kimuziki.
“Kwa sasa, Kenya ni kama imepoteza sauti yake maalum ya kimuziki. Haina utambulisho maalum kimataifa, kama ilivyokuwa katika miaka ya hapo nyuma. Tunahitaji kurejesha utambulisho wetu asilia, kama Tanzania invyotambuliwa kwa muziki aina ya Bongo Fleva,” akasema
Anasema kuwa ingawa mitindo mpya kama Gengetone na Urbantone imeibukia kuwa maarufu, vijana wanaotunga nyimbo hizo wanafaa kuwa na mwongozo maalum kutoka kwa kizazi cha wanamuziki waliotamba katika miaka ya hapo nyuma, ili kuhakikisha kuwa wanatoa miziki asilia.
“Miziki hiyo ni maarufu Kenya, ila bado haijapenya katika soko la kimataifa. Mafanikio ya muziki ni wakati unapata utambuzi Kenya na kimataifa. Ili kuirejesha Kenya ilipokuwa, kuna haja wanamuziki hao wa awali kuwapa mwongozo vijana wanaochipukia,” asema Bw Muchiri.