Mvunja mbavu Erico sasa aingilia ujenzi wa madaraja
NA FRIDAH OKACHI
MCHEKESHAJI Eric Omondi almaarufu ‘Erico’ anaendelea kumiminiwa sifa mtandaoni kwa kujitolea kujenga daraja mojawapo linalohatarisha maisha ya wakazi na wenyeji wa Kaunti ya Kisii.
Msanii huyo alichukua hatua ya kuchangisha fedha za kujenga daraja hilo baada ya video ya kutisha kusambaa katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ikionyesha jinsi msichana mdogo wa shule alivyorekodiwa akivuka kwenye daraja hilo wakati mto ulikuwa na maji mengi.
Kulingana na video hiyo, kijidaraja kibovu kimejengwa na mbao kuukuu, ni chembamba na kinaonekana dhaifu. Siku za hivi majuzi, Erico amegeuka kuwa mhisani.
Alisafiri hadi katika kijiji cha Nyakumbati, kumtafuta msichana huyo akiwa na lengo la kujenga daraja bora.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42, alisambaza video akiwa kwenye kivukio na baba ya mwanafunzi huyo, kuthibitisha hatari.
Katika chapisho lake, Yankee De +254, aliwatoa uzembe viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana wa Kisii Simba Arati na Mbunge Silvanus Osoro huku akiwataka waache malumbano ambayo hayasaidii mwananchi.
“Hii ni kazi ambayo Mabw Osoro na Arati wanafaa kufanya badala ya kupigana,” alisema Yankee De +254.
Vile vile mwakilishi wa wadi alinyoshewa kidole cha lawama, kwa kukosa kufahama matatizo ya wapigakura wake.
“Yaani jambo rahisi MCA wetu hawezi kutengeneza baada ya miaka 10 ya ugatuzi? Msanii amefika kujenga sasa,” aliandika Samuel Otachi.
Breshy Lynn alichangia kwenye chapisho hilo kwa kuhadithia jinsi alivyonusurika kupoteza maisha yake.
“Kulikuwa na daraja moja kama hii huko kwetu… Kufika ng’ambo ya pili (si mchezo)…,” alisema Breshy Lynn
Daraja hilo liko katika Mto Gucha katika Kaunti ya Kisii.
Harakati za Erico zinafanya baadhi ya watu kuhisi kuwa huenda msanii huyo anatafuta nafasi kuwa mwanasiasa.
“… Eric akisimama ugavana Nairobi dhidi ya Babu Owino, nampigia Eric mara 20,000 iwapo inaruhusiwa,” akasema Firstborn Wa Babake.
Naye Henry Henrik alitaka msanii huyo kuweka wazi iwapo anasaka namna ya kujitosa mazima kwa ulingo wa siasa.
“Eric Omondi, unataka kiti gani?” aliuliza Henry Henrik.