Mwanahabari Letoo akera wanamitandao kwa kuoa mke mmoja
NA FRIDAH OKACHI
WANAMITANDAO wameghadhabishwa na hatua ya mwanahabari Stephen Letoo kufunga ndoa na mke mmoja kinyume na mbwembwe zilizokuwa zimeenezwa mitandaoni atafunga ndoa ya mitala.
Mwanahabari huyo alifunga pingu za maisha na mpenzi wake Irene Renoi Kiptikoi kwenye kanisa la Methodist, Kaunti ya Narok kabla ya kuelekea kwenye uwanja wa Ole Ntimama.
Mmoja wa mashabiki alimlinganisha mwanahabari huyo na mwanafunzi ambaye hupiga kelele darasani, wengi wakifikiri kuwa hasomi vitabu. Na kusubiri kuanguka.
“Harusi ya Stephen Letoo ni mfano wa wale wanafunzi hupia kelele, na kukupeleka kulala mapema kisha asubuhi anaamka kusoma. Alafu anakuacha ukikoroma, mtihani ukija anapita. Unadhani alizaliwa mwerevu kumbe wewe ndo hutumii ubongo,” alisema shabiki huyo.
“Wanachama wa Men’s Conference mko na wanawake wangapi?” aliuliza.
Picha zilisambazwa mtandaoni zikionyesha kuwa amehalalisha ndoa yake na mke mmoja. Mashabiki walishangaa kuona picha hizo na kuuliza mbona akaoa mke mmoja licha ya kujenga taswira kuwa anashabikia ndoa za wake wengi.
Katika sherehe hizo katika uwanja huo wa Ole Ntimama, ulikuwa na wageni waalikwa zaidi ya 60,000.
Siku ya Ijumaa, mwanahabari huyo pia alifanya sherehe ya kitamaduni iliyofanyika Kilgoris ya kulipa mahali.
Kihistoria, ndoa za wake wengi hufanywa na tamaduni nyingi. Kwenye kitabu kitakatifu kwenye Agano la Kale, linaelezea mifano mingi ya matukio ya mitala. Katika Agano jipya ambalo madhehebu mbalimbali hutumia wakati wa kuhalalisha ndoa, linakataa desturi ya mitala na kushikilia ndoa ni ya mke mmoja pekee kama kanuni.