MWANAMIPASHO: Jirani pale Tanzania anatamba, amezindua tuzo kali za muziki, sisi huku?
NA MWANAMIPASHO
OYA Bwana! Hivi umesikia mikakati ambayo kamati andalizi ya tuzo za Tanzania Music Awards (TMA) 2024 zitakazotolewa Juni 14, imekuja nayo?
Nimemsikiza kwa makini sana naibu mwenyekiti wa kamati andalizi ya TMZ, Seven Mosha hadi nikaingiwa na tumbo joto.
Kwa nini sio Kenya? Hivi wana sisi tunakwama wapi. Wakati wenzetu ambao Kizungu kinawatatiza kweli kweli, wapo mbioni kuzipeleka tuzo zao kimataifa huku Kenya, wala hatuna tuzo za staa kwenye muziki.
Toka Kisima Awards zilizokuwa na mbwembwe zife, hakujawahi kuwa na tuzo zingine zenye shamrashamra.
Tumebakia na tuzo za filamu Kalasha Film and TV Awards ambazo ukiniuliza mimi naziona kuwa za kawaida sana maana kila mwaka zinafanywa kwa levo zile zile.
Mara ngapi tumewasikia washindi wakilalamika kutopokea fedha walizoahidiwa baada ya kushinda tuzo hizo?
Lakini tuachane na Kenya ambapo siku hizi tupo bize kushabikia kiki za kipuzi na maudaku mitandaoni, Tanzania kule wenzetu wanapiga mzigo kweli kweli.
Kule wanapatia uzito kabisa tasnia yao ya muziki. Na ndio maana siku zote hatutachoka kuishi kutamani showbiz ya kwao maana wao wanajua kufanya kweli.
Sasa kwenye tuzo hizi za TMA, kwa mara ya kwanza tena katika historia ya ukanda huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hafla ya utoaji tuzo hizo itapeperushwa mubashara na vyombo vya kimataifa MTVBase na BET.
Haijawahi kutokea kwamba vyombo vya kimataifa vikasadikika kuona thamani ya kusapoti kitu chetu Wana Afrika Mashariki mpaka imetokea hii.
Jamani sijui kama umenielewa?
Hivi sio vyombo vya habari tu, hivi ni vyombo vya habari vya kimataifa zaidi, ambavyo watu kama Jay Z, Beyonce wanaviheshimu.
Kwa maana hiyo, Watanzania pamoja na vigugumizi vyao kwenye kimombo, ndio hao wapo mbioni kujiongeza kujulikana kimataifa zaidi.
Lakini haiishi hapo tu, kwa TMA kufanikiwa kuwapata MTVBase na BET kuwa wadhamini wao wakuu wa matangazo ya hafla ya tuzo hizo, kuna mengi zaidi.
MTV na BET wamechagua vipengele sita ambavyo washindi wake watapelekwa kwenda kuhudhuria BET Awards nchini Marekani zitakazofanyika Juni 30 kule Los Angeles.
Kwa maana hiyo, sita hao watapata fursa ya kujichanganya na kubadilishana mawazo na mastaa wakubwa wa kimataifa. Aisee!
Wataweza kuhudhuria sio tu tuzo zenyewe, pre party, post party.
Na kwenye pati hizo, kutakuwa na fursa za wao kutumbuiza, sasa hapo kutakuwa na wadau wengi watajika kwenye dunia ya muziki na chochote kinaweza kutokea kwa mtu kuishia kutambuliwa au kusainia au kuchukuliwa na lebo au mdau mkubwa wa burudani kwa ajili ya kufanya biashara za muziki kimataifa.
Nimemsikiza Mosha ambaye anafanya kazi Sony Music, akisema kuwa kila mara wanapokaa kwenye vikao, stori nyingi kuhusu soko la muziki Afrika ambazo huangaziwa sana huwa ni kuhusu mataifa ya Nigeria na Afrika Kusini kwa kuwa masoko yao tayari yamekaa vizuri.
Mosha anasema vitu hivi vimekuwa vikimwingia sana na akawa anawaza na lini Tanzania wataweza kufika levo za kuzungumziwa kihivyo.
Leo hii yeye na kamati yake wameanza kupiga hatua tena hatua kubwa. Wanasapotiwa mpaka na Wizara ya Utalii, jambo ambalo sijawahi kuliona Kenya.
Ndoto ya Mosha ni kuzifikisha tuzo hizi kwenye levo ya Trace Music Awards, MTV Music Awards, BET Awads ambazo huwa sio hafla za mchezo wewe.
Hapa najikuna upara najiuliza Kenya ni lini? Au tumalizane kwanza na mambo ya mbolea feki?