DOMOKAYA: Katika ndoa za maceleb, nyuma ya pazia kuna vijimambo kama ndoa zingine tu
NA MWANAMIPASHO
WANGWANA walishatuambia miaka ile, “lisemwalo lipo na kama halipo basi lipo njiani laja”.
Mwaka jana nipo kijiweni, anatokea mwana na kuanza kunipakulia maukoko ya stori za mjini.
Ananiambia unaiona ile ndoa yake Pascal Tokodi na Grace, ile naipa kama sana miaka miwili.
Najua mwana wangu ni mmbea, na si mmbea tu, ni mmbea sana. Namwangalia na kumkashifu kwa kuwatakiwa watoto wa wenyewe nuksi.
Mbona naona wanaposti picha na video za kichokozi. Namuuliza mwana. Anaguna na kuniambia, mpumbavu wewe usiamini kila kitu ambacho macho yanaona pale hamna ndoa.
Nikamhoji mwana zaidi, nikataka kufahamu taarifa zake kazitoa wapi maana haishi na wale maceleb ila wana ukaribu tu.
Akaniambia, pamoja na wao kuposti maisha ya kutamanisha na kumfanya kila mmoja kuitamani ndoa, yule Pascal kila mara anapopata muda hukimbia kwake kumlilia jinsi ndoa inavyompeleka kasi.
Nami nikamjibu, si ndio maisha lakini Sheikh. Akanikaripia kwa ukali, “huelewi wewe kinachoendelea.”
Kweli wakati niliamini itakuwa ni misukosuko ya ndoa, kumbe yalikuwepo mengi zaidi.
Haikuwa misukosuko ya kawaida.
Ishu ni kwamba wanandoa hao walikuwa wanahangaikia kuishi maisha ya staha na kifahari wakati mtaji ndio hawana wa kutosha.
Kibaya hata zaidi kwa mujibu wa stori iliyochapishwa na Nairobi News, ni kwamba kwenye ndoa ile mwenye riziki alikuwa ni mmoja Pascal, huku bibiye akiwa ni mke nyumbani.
Kwa maana hiyo majukumu yote ya kuishi maisha hayo yalimwangukia Pascal ambaye hakika alijitahidi sana kuipambania familia yake kuishi maisha yale ya kutamanisha.
Lakini hela zilipoanza kumpiga chenga, ndoa ikageuka na kuwa chungu. Mwisho wa siku wakashindwa kuvumiliana na ikawa bora kila mmoja ashike hamsini zake. Ndio maisha ya mastaa wetu hawa.
Kwa kututengeneza pale mitandaoni, hawashindwi lakini kumbe nyuma ya pazia, wenzetu wanahangaika na maisha kama sisi tu.
Lakini Sheikh faida ya kufeli maisha ni nini haswa?