Njeeri akiri kuachana na Muigai wa Njoroge
NA WANDERI KAMAU
MKEWE mwanamuziki wa nyimbo za Injili na kuishauri jamii mwenye ufuasi mkubwa eneo la Mlima Kenya John Muigai Nyururu almaarufu Muigai wa Njoroge, Bi Njeeri wa Muigai, amekiri kwamba waliachana kitambo baada ya kushindwa kusuluhisha tofauti zao za ndoa.
Mnamo Alhamisi, Bi Njeeri alisema walifikia uamuzi huo baada ya kusuluhisha na kuiokoa ndoa yao bila mafanikio.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, Bi Njeeri alieleza kwa kina changamoto nyingi na mahangaiko ya kimawazo aliyopitia kwa muda mrefu, hasa baada ya kufahamu kuwa mumewe alikuwa ashapata mke wa pili.
“Tulijaribu. Sitaki kumlaumu mtu yeyote. Tulijaribu, lakini hatukufanikiwa. Ni jambo la kuhuzunisha. Ghadhabu ni kama ajali. Niliona sababu ambazo huwafanya watu kuuana. Tulisukumana sana na tukaona kuwa ndoa yetu haiwezi kufaulu tena,” akasema Bi Njeeri.
Wawili hao walioana mnamo 2008, baada ya kukutana wakati Bw Muigai alikuwa kwenye hatua za mwanzo katika safari yake ya muziki.
Wakati huo, Bi Njeeri alikuwa akihudumu kama mjakazi katika makazi yaliyokuwa karibu na mahali ambapo mwanamuziki huyo alikuwa akikaa.
“Tulioana bila kuambiana chochote. Tulipendana tu na kuanza maisha jinsi tulivyokuwa,” akasema Njeeri.
Kwenye mahojiano hayo, alieleza jinsi aliamua kuingilia ulevi kama njia ya kujiliwaza kutokana na matatizo waliyokuwa wakipitia.
Alisema kuwa watoto wake walihangaika pakubwa kutokana na hali ngumu ya kimaisha aliyokuwa akipitia.
Muigai wa Njoroge ni miongoni mwa wanamuziki wachache wenye ufuasi na umaarufu mkubwa katika eneo la Mlima Kenya, kutokana na utunzi wake wa kipekee wa nyimbo.
Baadhi ya nyimbo zake zinazofahamika na wengi ni ‘Kigutha’ (Kiboko), unaorejelea athari za ugonjwa wa Ukimwi na virusi vya HIV.
Mwanamuziki huyo alikuwa miongoni mwa wale waliotunga nyimbo za kumuunga mkono Rais William Ruto na mrengo wa Kenya Kwanza kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Kama njia ya kumrejeshea mkono, Rais Ruto alimteua kama mwanachama wa Bodi ya Kuainisha na Kusimamia Filamu Nchini (KFCB).
Wiki iliyopita, Njeeri alikiri kwamba ilimchukua miaka mitano kuamini kwamba mumewe alikuwa ashamwoa mke wa pili, anayeitwa Queen Stacey.