Bambika

Pasta Ng’ang’a ‘atoa makucha’ EACC ikimwandama kuhusu ardhi ya Kanisa

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MVUTANO baina ya Pasta James Ng’ang’a na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) unaendelea kutokota kuhusu umiliki wa ardhi alikojenga kanisa lake.

Tayari, mhubiri huyo wa kanisa la Neno Evangelism Centre, Nairobi amejitokeza wazi na kusema kuwa yuko tayari kutetea ardhi hiyo, akisema aliinunua kwa njia halali kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) mnamo 2004.

Kaasisi huyo pia amedai ana hatimiliki halali ya ardhi hiyo, akishikilia ni ya 1980.

“Nasikia EACC ikisema nimenyakua ardhi hii. Hatimiliki ya ardhi hii ni ya 1980, ila ikatoka 1992. Nilinunua ardhi hii 2004. Halafu mnasema mimi nilinyakuwa ardhi hii. Hayo ni maswali mnayofaa kueleleza kwa CBK, maanake ndiyo iliniuzia. EACC inafaa kwenda kwa Wizara ya Ardhi. Mimi huwa sitoi hatimiliki za ardhi. Acheni sarakasi, kwani mnataka kuiharibia serikali jina. Mimi niliangalia uhalali wa hatimiliki hiyo,” akasema.

Akaongeza: “Hatimiliki hii imekuwa halali tangu enzi ya marais wastaafu (marehemu) Daniel Moi, Mwai Kibaki na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta. Wakati huo wote, EACC ilikuwa wapi?

EACC imewasilisha kesi mahakamani ikiitaka kuipa kibali kutwaa vipande vitano vya ardhi, inavyodai vilinyakuliwa na wawekezaji wa kibinafsi.

Miongoni mwa watano hao walioshtakiwa na tume hiyo ni Pasta Ng’ang’a.

Vipande hivyo vya ardhi viko katika makutano ya barabara ya Haile Selassie na Uhuru Highway.

EACC inadai kuwa ardhi hizo zina thamani ya Sh1.6 bilioni, na zilikuwa zimetengewa Shirika la Reli Kenya (KRA), kabla ya kunyakuliwa na wawekezaji wa kibinafsi.

Wale walioshtakiwa na EACC kuhusiana na ardhi hizo ni Makamishna wa zamani wa Ardhi, Mdhamini Aliyesajiliwa wa Neno Evangelism Centre, Pasta James Maina Ng’ang’a, Arts 680 Limited na Kobil Petroleum Limited (Rubis Energy).

Pasta Ng’ang’a na kanisa la Neno Evangelism wameshtakiwa kuhusiana na vipande vya ardhi nambari LR. No. 209/9640 na LR. No. 209/12361 vyenye thamani ya Sh480 milioni na Sh30 milioni mtawalia.