Sepetu aelezea sababu za kuzuiwa kuingia Ikulu wakati wa uzinduzi wa albamu ya Harmonize
NA SINDA MATIKO
BAADA ya mwigizaji staa Wema Sepetu kulia kutoruhusiwa kuingia kwenye uzinduzi wa albamu ya Harmonize iliyohudhuriwa na Rais Samia Suluhu hivi majuzi, ufafanuzi umetolewa.
Sepetu alielezea kusikitishwa kwake baada ya walinzi wa Ikulu kumzuia asiingie kwenye uzinduzi huo.
Na hata baada ya kuwasihi walinzi wamruhusu, hakukubaliwa.
“Nimesikitika kwa sababu nimefika hapa saa tatu kasoro mama (Rais) tayari alikuwa yuko ndani. Sijaweza kupata mama ameongea nini maana nilikuwa nje.”
Baada ya lalama zake, maelezo kutoka kwa Harmonize yalifafanua sababu za Wema kuzuiliwa.
Imefahamika kuwa Wema ambaye alialikwa na Harmonize hakufuata masharti na kanuni walizopewa waalikwa.
Siku moja kabla ya uzinduzi huo kufanyika, Harmonize aliwakumbusha waalikwa wote kuwa wafanye hima wawahi kuingia ukumbini kabla ya Rais sababu kutakuwepo na mabadiliko ya kiitifaki Rais Samia akishaingia ukumbini kwani watu wengine hawataruhusiwa ndani baada ya Rais.