Si lazima ujengewe nyumba ‘ushago’, mke wa pasta Ezekiel ashauri wanawake
NA FRIDAH OKACHI
WANAWAKE wengi nchini huwa na msukumo wa kutaka kujengewa nyumba vijijini hata kama wanaishi mijini na waume wao.
Makao hayo yakitumika wakati familia inaenda likizo au shughuli ya dharura inapotokea pale nyumbani mashinani almaarufu ‘ushago’.
Lakini mke wa Pasta Ezekiel Odero, Bi Sarah Wanzu, ana mtazamo tofauti kabisa, akishikilia nyumba inaweza kuwa ni kuta tu na paa lakini msingi wa ndoa uko kwa mume na mke kuonyeshana upendo na ucha-Mungu.
Kwake kujengewa nyumba kijijini si suala la kupewa kipaumbele.
Sarah amewataka wanawake waache kuwasukuma waume wao kujenga nyumba vijijini.
Katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la New Life eneo la Mavueni, Kaunti ya Kilifi, alisema ndoa sio tu kujenga nyumba yako mwenyewe.
“Hatuna nyumba kule ambako nimeolewa. Tukifika huko, gari ndilo hugeuka kuwa nyumba yetu. Pastor Ezekiel ndiye kifungua mimba na sijalilia nyumba,” akasema.
Mama huyo wa watoto watatu aliwataka wanawake kuzingatia mambo ya maana na kuacha kulalamikia waume wao kwamba wanataka kujengewa.
“Nyumba sio ndoa na nyumba sio maisha. Mimi sijajengewa. Je, ukijengewa na uachwe, hiyo nyumba nani atakaa humo?”aliuliza.
Mhubiri huyo alisema anachotaka ni maisha yenye afya na nguvu zaidi za kumtumikia Mungu.
Sarah alisema licha ya kuwa hajasoma sana, anataka kuhubiri injili ya Mungu duniani kote.
Ndoa ya Sarah na Pasta Odero haijakuwa na siri sana.
Mwaka 2023 pasta huyo alidai kuwa mkewe anajua PIN yake ya M-Pesa katika simu yake.