Ssaru adai muziki ‘mchafu’ unamwingizia posho kuliko ule wenye maadili
Na RAJAB ZAWADI
RAPA mwenye uwezo wa kuimba vile vile Sylvia Ssaru almaaarufu Ssaru wa Manyaru kadai sababu zake kupenda kutunga nyimbo chafu, kumechangiwa pakubwa na Wakenya.
Lakini kubwa hata zaidi Ssaru anasema amegundua muziki mchafu ndio unaomwezesha kutengeneza posho la kisawasawa tofauti na pale anapotunga nyimbo zenye maadili.
Kulingana naye, kila anapoachia muziki mzuri huwa haufanyi vizuri akilinganisha na muziki mchafu.
Akitolea mfano, Ssaru ameitaja hiti yake ya Kaskie Vibaya kuwa moja ya kazi zake chafu zilizomwigizia hela ndefu mwaka jana kando na kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii ikiwemo kukashifiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la muziki la wasanii Wakenya MCSK, Dkt Ezekiel Mutua.
Mutua alimchamba Ssaru kwa kuachia wimbo usiokuwa na tija wala maadili akiutaja kuwa muziki potovu usiokuwa wa manufaa kwa jamii.
Lakini kwa kumjibu, Ssaru alimtaka Mutua aliyesifika kwa kuzifungia nyimbo chafu alipokuwa bosi wa bodi ya filamu nchini KFCB, kuwalaumu Wakenya.
“Mwanzo kabisa kwenye runinga zetu tunaona kila siku nyimbo chafu za wasanii wa nje zikipigwa lakini tunapozifanya sisi wasanii wa nyumbani inakuwa ishu. Lakini kubwa zaidi pia muziki msafi wa wasanii wa nje zinachezwa sana vile vile huku kwetu, ila sisi tukifanya miziki kama hiyo, hatuchezwi. Lakini tukiachia miziki inayochukuliwa kuwa chafu kama Kasikie Vibaya, mapokezi yanakuwa ni makubwa sana na mapokezi yanapokuwa makubwa naishia kupata shoo nyingi sana na kwa maana hiyo natengeneza hela ya kutosha,” anafafanua Ssaru.
Kwa utathmini huu, Ssaru anasema amekuja kugundua na kuamini kitu kimoja.
“Kuwa Wakenya wanapenda miziki michafu nasema hivi kwa sababu pia nimeachia nyimbo zingine zinazoweza kuchukuliwa kuwa safi. Nilianya rhumba ya Ssaru, nikaachia dancehall lakini mapokezi yamekuwa ya kusua sua tu sasa kwa nini nisiendelee kutunga muziki ambao watu wanaupenda” Ssaru anahoji.
Kasikia Vibaya aliyoiachia miezi tisa iliyopita imetizamwa mara zaidi ya milioni 10 kwenye YouTube.