Stephen Letoo aachana na kitimoto cha Men’s Conference
NA FRIDAH OKACHI
MWANAHABARI Stephen Letoo baada ya kuona yanayojadiliwa mitandaoni, ameamua kuweka zingatio kwa kuitunza ndoa yake mbichi kabisa, akisema amejiuzulu uenyekiti wa Men’s Conference, jukwaa la kutetea haki na masilahi ya wanaume katika jamii.
Bw Letoo alipata msukumo kutoka kwa wanachama wa Men’s Conference.
Hata hivyo, ametoa wito kuwa atakayechukua nafasi hiyo ajue haitakuwa rahisi kwani hata yeye ilimbidi kutia bidii zaidi ndiposa akatoshea kwa vyatu vya mtangulizi wake, marehemu Mzee Jackson Kibor.
Bw Letoo alisema kuwa aliafikia uamuzi huo kutokana na kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uongozi wake.
“Baada ya kutafakari na kuoana yanayoendelea mitandaoni, nimeamua kujiuzulu kama mwenyekiti. Na hivyo, nimewasilisha barua yangu ya kujiuzulu katika ofisi hiyo jijini Nairobi,” alisema Bw Letoo.
Mwanahabari huyo alisema anaondoka kwa ofisi hiyo mara moja baada ya kufanya majadiliano ya kubadilishana fikra na marafiki na wandani wake wa karibu kote duniani.
Aliwataka wanachama wa Men’s Conference kumtafuta kaimu mwenyekiti.
“Nimewaruhusu wanachama wenzangu kutafuta kaimu mwenyekiti, ambaye anaweza kuja kwangu kwa mashauriano yoyote,” aliongeza.
Alionya kuwa wadhifa huo sio wa watu walio na mioyo dhaifu.
“Ulikuwa uamuzi mgumu sana kujaza nafasi ya Mzee Kibor. Na ninaweza kuwahakikishia wanachama kwamba kiongozi ajaye atakuwa na kibarua kigumu kutoshea kwa viatu vya mimi Stephen Letoo,” akaeleza.
Hata hivyo, alitoa wito kwa mrithi wake kuendelea kupigania haki za mtoto wa kiume.
Alisisitiza kuwa atasalia kuwa mwanachama wa vuguvugu la Men’s Conference baada ya kushikililia nafasi hiyo kwa takriban mwaka mmoja na nusu.
Kabla ya kufunga ndoa na mkewe, wengi walikuwa na matarajio angeingia kwa ndoa ya kuwa na wake wengi.