• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Stivo Simple Boy: Nilivalia jeans ya Kiafrika ya Sh237,600 kurekodi muziki

Stivo Simple Boy: Nilivalia jeans ya Kiafrika ya Sh237,600 kurekodi muziki

NA FRIDAH OKACHI

RAPA Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy ameibua gumzo mtandaoni baada ya kuonekana akiwa amevalia nguo ambazo zilitengenezwa kwa kitambaa cha jeans aina ya Denim na kupambwa Kiafrika.

Sababu yenyewe aliyotoa ya kuvalia vazi hilo la kipekee iliwavunja mbavu mashabiki wake katika mitandao ya kijamii.

Msanii huyo aliambia Taifa Leo vazi hilo spesheli lilimgharimu Sh237,600 (USD 1800) na alilivaa akiingia studioni kurekodi vibao vipya.

Hii inamaanisha kuna kitu ambacho anakipika jikoni, akiwataka mashabiki wa muziki wake kukaa mkao wa kula.

“Sivai vazi tu hivihivi, hapana. Hii Denim ya Kiafrika ni brandi na tuliwahusisha wataalum wa mtindo wa mavazi waliopendekeza nivalie hivi,” akasema Stivo Simple Boy.

Kwa mwonekano, vazi hilo ni kama sweta iliyoshonwa na kuunganishwa na kipande cha jeans.

Stivo Simple Boy alisema vazi hilo linaandamana na ngoma mpya ambayo aliomba mashabiki wake kuwa na subira kwa sababu “nitaipakia mtandaoni hivi karibuni”.

“Nilitaka vazi ambalo bila shaka linaandamana na wimbo wangu. Niliwaambia wale wataalum wa mavazi ile ngoma yangu jinsi ilivyo na wao wakaitafsiri jinsi inavyohitajika,” alieleza.

Alifichua kidogo kuhusu mojawapo ya ngoma hizo zake.

Japo alitaja anwani, alisema ni muhimu kuvuta subira kiasi kabla ya kutambulika.

“Ngoma hii mpya nimerekodi mtindo wa secular,” akasema kumaanisha si wa kidini.

Kufichua siri kiasi tu, ni muziki wenye maudhui ya masaibu yaliyomwandama mwanamuziki huyu kabla na baada ya kuanguka wakati wa kuburudisha mashabiki wake.

Mbunifu wa mtindo wa vazi hilo Bw Maxwell Kin kutoka kampuni ya Diesel RKO Design, alisema vazi hilo ambalo si la kawaida huvaliwa kwenye sherehe maalum na iwapo utalivalia, linawaacha mashabiki na watazamaji vinywa wazi.

“Mtindo ni wa Demin ambao umechanganywa na uzi. Mtindo huo unavaliwa na watu maarufu duniani,” alieleza Bw Kin.

Bw Kin alidai kuwa mtindo ambao msanii huyo alivalia, ilikuwa ni mbinu ya kuleta mshangao na wakati huo huo, kulenga kuleta ufahamu kwa mashabiki.

“Vazi hilo linauzwa kwa bei ghali mno maana linaleta ufahamu fulani wakati unapolivalia. Wakati wa kushona vazi hilo, huhitajika ubunifu mwingi tena wa hali ya juu,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Magavana wa zamani kusomewa ‘dhambi’ zao mbele...

Ruto ajibu maswali ya mbolea feki ziarani Amerika

T L