• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Tulimalizana na Raila kiungwana, hatukufika mahakamani – Sauti Sol

Tulimalizana na Raila kiungwana, hatukufika mahakamani – Sauti Sol

Na SINDA MATIKO

KAMA utakuwa unakumbuka, Mei 2022 taifa likiwa linakaribia Uchaguzi Mkuu, bendi ya Sauti Sol iliiba vichwa vya habari baada ya kutangaza kwamba itaichukuliwa hatua za kisheria mrengo wa siasa wa Azimio unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Ishu ya Sauti Sol na Azimio ilihusiana na matumizi ya hiti yao Extravangaza kwenye mojawepo ya heka heka zao za kisiasa za kujipigia debe kuelekea uchaguzi huo.

Kwenye hafla ya uzinduzi wa Mgombea Urais mwenza, Bw Odinga pale KICC, ambapo Martha Karua alitangazwa kuwa mgombea mwenza, Azimio waliucheza Extravangaza wakati wakimzindua rasmi Bi Karua.

Ishu hii haikukaa sawa na Sauti Sol na muda si mrefu wakatoa taarifa ndefu wakisisitiza kuwa ni lazima watachukua hatua za kisheria kwani walichofanya Azimio ni uvunjaji wa matumizi ya haki miliki yao kwa maana ya kutumia wimbo wao kujipigia debe pasi na kupata ruhusa kutoka kwenye bendi hiyo.

Sauti Sol walisisitiza kuwa kando na kutumia wimbo wao kujifaidisha, Azimio ilichora taswira kwa umma kwamba bendi hiyo inaunga mkono mrengo huo wa kisiasa jambo ambalo kwao sio kweli.

Ni sakata ambayo ilizua tumbojoto na kuangaziwa na vyombo mbalimbali vya habari. Azimio kwa upande wake ilijaribu kujitetea kwa kusema kwamba ilipata wimbo huo kutoka kwa chama cha wanamuziki cha MCSK ambacho Sauti Sol ni wanachama.

Baada ya matukio hayo, wengi huenda wakawa wanaamini kuwa tayari kesi hiyo ipo mahakamani.

Kwenye pekuapekua  zetu, Taifa Leo Dijitali ilipiga stori na wakili wa bendi ya Sauti Sol Moriasi Omambia kuelewa ishu hiyo imekaaje.

“La hasha hatukufika mahakamani. Ninachoweza kusema ni kwamba utata huo tuliumaliza kiungwana nje ya mahakama. Tulifanya vikao na majadiliano ya kina na Paul Mwangi ambaye alikuwa ndiye katibu wa Azimio na tukayamaliza kwa kuwapa elimu na ufafanuzi wa kwa nini ni hatia kutumia haki miliki za watu kwa manufaa yao bila ya idhini zao hata ikiwa haki miliki hizo zipo nje kwenye hadhara,” Omambia alieleza.

Tulipombana sana kutaka kujua kama Azimio iliwarubuni Sauti Sol kwa kuwafidia kwa kitendo hicho, Omambia aligeuka mbogo.

“Masuala ya hela siwezi kusema ila kama nilivyokueleza hapo awali tulimaliza utata huo kiungwana. Tuliwapa darasa kuhusiana na haki miliki na kwa nini hata hao MCSK wanaodai kuwa na nguvu za kupeana nyimbo za wasanii nao walivunja sheria. Kuhusu masuala ya fidia ama nini naomba nisizungumize hilo.”

Aidha, Omambia alikana kufunguka ishu ya kushtakiwa na Seneta Crystal Asige aliyekuwa kwenye lebo ya Sol Generation inayomilikiwa na Sauti Sol.

“Ishu hiyo siwezi kuizungumzia maana ipo mahakamani na itakuwa ni makosa kuijadili wakati ikiwa ni kesi inayoendelea.”

  • Tags

You can share this post!

Lizzie Wanyoike alivyonusurika kifo 1960

Athari za El Nino Mukuru-Kayaba

T L