• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Usimpe mke presha ya kukuzalia kijanadume – Nameless

Usimpe mke presha ya kukuzalia kijanadume – Nameless

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI David Mathenge almaarufu Nameless amesema presha za mashabiki kwamba yeye na mkewe Wahu walitarajia mtoto wa kiume hazina maana kwani la muhimu ni afya ya mama mjamzito na mtoto anayembeba tumboni.

Nameless alifunguka jinsi alivyoepuka shinikizo kuhusu jinsia ya mtoto wakati mkewe alikuwa amebeba ujauzito wa kitinda mimba wao.

Msanii huyo alisema kuwa licha ya kupokea jumbe na maoni kibao kutoka kwa wanamitandao kuwa walitarajia kuwa angepata mtoto wa kiume, tayari walikuwa–Nameless na mkewe–wamefanya vipimo vya kuhakikisha wanatarajia mtoto wa kike kabla ya kutangaza hadharani ujauzito huo.

Alisema uvumi ulienea mitandaoni, mashabiki wengi wakitabiri kupata mtoto wa kiume.

“Tulipotangaza kuwa tunatarajia mtoto, tulijua tunatarajia mtoto wa kike. Hata karibu kila mtu alipokuwa akituambia alijua kuwa atakuwa mtoto wa kiume, sisi wenyewe tulitulia tuli,” alisema Nameless.

Kwenye mahojiano, Nameless alibaini kuwa lengo lao kama wazazi kwenye safari hiyo muhimu lilikuwa afya ya mama na mtoto badala ya jinsia.

“Kwa kweli haikuhusu kama ni mvulana au msichana. Ilikuwa ni kuhusu mtoto mwenye afya njema,” alisisitiza Nameless.

Baba huyo wa mabinti watatu, amethibitishia ulimwengu kuwa kupata watoto wa kike pekee hakumdunishi na pia, watoto wa kike hawapunguzi jukumu lake kama mzazi.

“Kila mtoto ni sawa machoni mwa wazazi. Kwetu sisi tulifurahi kwamba kifunga mimba wetu alikuja akiwa mzima. Na yeye ndiye nyota, mrembo anayeng’aa. Huwa nafurahi sana kuwa baba wa wasichana,” aliongeza.

Wikendi iliyopita, familia ya Bw Mathenge ilipata dili ya ubalozi wa nepi za mtoto (diapers).

Alisistiza umuhimu wa majukumu ya wazazi kwa kuruhusu picha za mwanawe kutumika.

“Niliamua picha yake itumike kwa sababu nataka kupitisha ujumbe kwamba kulea mtoto si tu suala la mwanamke bali ni suala la wazazi wote wawili kuwepo katika maisha ya watoto wao,” alifafanua.

Wakati wa kutia saini dili hiyo, mkewe Rosemary Wahu alionyesha furaha yake, akisema ni safari ya ushirikiano na mumewe.

“Kushirikiana na kampuni hiyo ya nepi imekuwa safari nzuri sana. Waliunga mkono onyesho letu la uhalisia la This Love, na tumejenga uhusiano thabiti pamoja. Nimefurahi kufanya kazi nao,” alisema Wahu.

  • Tags

You can share this post!

Raila, Ruto watofautiana kuhusu ubadilishaji matokeo

Murkomen ashikilia hakuna jipya takwimu za ajali

T L