• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Waithaka wa Jane adai kwa muziki, wengi huzimiana nyota

Waithaka wa Jane adai kwa muziki, wengi huzimiana nyota

NA MWANGI MUIRURI

WAITHAKA wa Jane ambaye mashabiki wengi humtawaza kama Mfalme wa Mugithi kwa kumsawiri kama aliyemwondoa Samidoh kutoka nafasi hiyo, sasa anadai kwamba sekta hiyo ya usanii imejaa watu wenye wivu.

Haya yamejiri huku mashabiki wake wanaoishi ughaibuni wakilalamika kwamba kuna msanii hapa nchini ambaye kwa ushirikiano na wanasiasa fulani, huhakikisha Waithaka wa Jane hapati viza za kumwezesha kutua kwa baadhi ya mataifa kuandaa shoo.

“Tunachunguza kupitia mabalozi kadha wa huku Ulaya. Tunataka kujua ni kwa nini wasanii ambao wameiva na wako na ufuasi mwingi huku wakimtaka Wa Jane huwa ananyimwa viza. Ni suala hata ambalo tunatafakari kumwandikia Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Bw Musalia Mudavadi,” akalalama Sophia Williams mnamo Januari 1, 2024.

Ng’ambo wakiteta, Wa Jane ameshikilia kwamba masaibu mengi ndani ya usanii ni kisa cha ‘kikulacho ki nguoni mwako’.

“Kile kinachotumaliza sisi wasanii ni wivu. Kuna baadhi miongoni mwetu ambao hawataki kuona wenzao wakipaa kwa ufanisi. Kazi tu ni kuzimiana nyota,” akasema Wa Jane.

Akisema kwamba wasanii wengine huwa katika kazi ya kuwaguguna wasanii wenzao hadi waishe, alisema katika ujumbe wake wa kufunga mwaka kwamba hali hiyo imeifanya sekta ya ubunifu wa sanaa ikose mvuto na ulezi wa vipaji.

“Lakini niwape moyo kulingana na hali yangu binafsi… Walio na wivu hawatawahi kukuzimia nyota kwa kuwa mwenye kupeana baraka ni Mungu. Wanapokosa usingizi wakikupangia njama ya kukumaliza, Mungu katika kiti chake cha enzi huwa anasimama na wewe na mwisho wa ubaya wao huwa aibu,” akasema.

Wa Jane ambaye hufahamika sana kwa jina ‘Karaiku’, na ambaye ametoka katika familia ya ndugu wengine watano wasanii kutoka kijiji cha Kiriaini katika Kaunti ya Murang’a alisema “wenye kinyongo na wivu waelewe huwa wanabishana na Mungu ambaye ndiye mgavi wa fanaka za maisha”.

Mwanamuziki Waithaka wa Jane (kulia) akiwa na Muthoni wa Kirumba. PICHA | MWANGI MUIRURI

Aliongeza kwamba yeye atazidi kuzingatia imani kwa Mungu huku akipalilia husiano zake na mashabiki wake kwa kuwa ufanisi wake umehifadhiwa hapo.

“Cha maana kwa wasanii pia ni wajichunge na anasa potovu, wajaribu kuwekeza na wazingatie msaada kwa jamii wakati Mungu amewabariki,” akasema.

Alisema anaruka mwaka akiwa na matumaini tele kwamba atapaa zaidi katika maisha yake ya usanii na ya kibinafsi na kwamba Wakenya watapata afueni ya kiuchumi kuwawezesha kujitokeza katika shoo zake na kumwachia mihela.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mvua kuendelea kushuhudiwa maeneo mengi nchini –...

Ubomoaji wa nyumba za maskwota 3,500 waanza Msambweni

T L