Wakenya kulipa Sh15,000 kupata kibali kupiga shoo Tanzania
NA SINDA MATIKO
MSANII yeyote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayetaka kuenda kupiga shoo au kufanya kazi ya sanaa nchini Tanzania sasa atatakiwa kulipa Tsh300,000 (Sh15,000) kupata kibali.
Haya ni kwa mujibu wa maelekezo mpya kutoka kwa Baraza La Sanaa Tanzania (BASATA) ambalo limeamua kupunguza ada ilizokuwa ikitoza kwa wasanii wa nje kufanya shoo Tanzania.
“Kwa kanuni iliyokuwepo, inasema kwamba msanii yeyote kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeingia nchini kufanya kazi za sanaa atalipa Tsh1 milioni (Sh51,000) na ambaye anatoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki atalipa Tsh1.5 milioni (Sh77,000),” anasema Katibu Mkuu wa BASATA Kedmon Mapana.
“Kanuni hiyo vile vile haijazungumzia makundi au bendi, tuseme kwaya kutoka Burudi inaingia nchini au labda Koffi Olomide anaingia na madansa wake 20 ilikuwa kwamba kwa kila kichwa kinalipa Tsh1 milioni. Lakini tukahoji basi yule msanii atakuwa anafanya biashara gani,” ameongeza.
Kwa msingi huo, Mapana anasema BASATA imeamua kufanya marekebisho ya sheria hiyo ili kuwachochea wasanii zaidi kwenda kufanya kazi za sanaa Tanzania.
“Kuanzia Juni, kanuni inasema kuwa kundi au bendi ya msanii inayoingia Tanzania basi kitalipa Dola 500 (Sh66,000) tu. Kwa msanii pekee anayetoka ndani ya EAC sasa atalipa Tsh300,000 na kwa anayetoka nje ya EAC atalipa Tsh500,000 (Sh26,000). Lengo letu kama BASATA ni kuwa kichocheo kwa wanaojishughulisha na masuala ya burudani na wala sio kikwazo. Kwa maana hiyo, tunataka wanaojishughulisha na sanaa waweze kuwaleta wasanii wengi zaidi Tanzania,” ameongeza Mapana.
Kwa muda sasa, wasanii Watanzania wamekuwa wakilipia ada kubwa ya vibali wanayotozwa na BASATA kila wanapoandaa matamasha ndani ya nchi au hata pale wanapotaka kwenda kupiga shoo nje za nchi.
BASATA inasema mchakato huu ambao sasa umetolewa kwa wasanii na umma kwa ujumla nao kutoa mapendekezo yao, unalenga kuondoa kero hizo lakini pia kuhakikisha inalinda soko la muziki wa Tanzania kwa faida ya msanii wa Kitanzania.
Tofauti na Tanzania, hazipo ada zozote ambazo hutozwa hasa wasanii wa muziki wanaoingia Kenya kufanya kazi za muziki.
Ila zipo ada zinazotozwa wanaoingia nchini kwa ajili ya kujihusisha na sanaa ya filamu.