Bambika

Wanafunzi Moi wakubaliana na sheria ya kuzima vimini

February 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

KAULI kwamba ‘vazi langu ni chaguo langu’ haina nafasi katika Chuo Kikuu cha Moi kufuatia hatua ya usimamizi wa chuo hicho kupiga marufuku wanafunzi kuvaa nguo zinazoonyesha maumbile ya ndani.

Mnamo Februari 6, 2024, chuo hicho kilitangaza marekebisho ya sheria zilizo katika katiba ya taasisi hiyo kama sheria na kanuni zinazoongoza maisha ya wanafunzi katika taasisi hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo, uongozi wa chuo hicho umetoa kanuni kali ya mavazi wanayostahili kuvaa wanafunzi wanapokuwa ndani ya chuo.

Katika tangazo lililotolewa Jumanne, mkuu wa maswala ya wanafunzi Alice Mutai, alisisitiza kuwa hakuna nafasi kwa wanafunzi wanaovaa nguo wazi.

Dkt Mutai aliambia Taifa Leo kwamba si jambo geni kwani sheria kuhusu mavazi ipo katika sera na sheria zinazosimamia taasisi hiyo na kila mwanafunzi anayejiunga na chuo hicho hupewa sheria hizo.

“Hakuna jipya ambalo tumefanya, tunasisitiza tu sheria ambazo zimekuwa zikitumika shuleni kupitia toleo la saba la makala ya sheria zetu,” Dkt Mutai alisema Alhamisi.

“Ningependa kukujulisha Kifungu cha 3.1.1 a, c, d na e cha Sheria na Kanuni zinazoongoza Maadili na Nidhamu ya Wanafunzi. Wanafunzi wanatarajiwa kuvaa mavazi ya heshima na mavazi yanayofaa, yale ambayo tumeona hivi majuzi ni aibu hasa uvaaji usiofaa wa baadhi yenu,” sehemu ya notisi hiyo ilisema.

Hatua hiyo imepongezwa na baadhi ya wanafunzi wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wanafunzi wa Chuo hicho Cornelius Kipkoech.

“Hatua hiyo ilichelewa… baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitembea chuoni wakiwa nusu uchi. Tabia hii imesababisha baadhi yetu kukosa umakini darasani, hasa wanafunzi wa kike wanapofika darasani wakiwa wameweka wazi miili yao kwa kuvaa nguo zisizokuwa na siri,” alisema Bw Kipkoech.

Aliongeza kwamba agizo hilo litarejesha hadhi miongoni mwa wanafunzi pamoja na kukomboa taswira ya chuo hicho kwa waajiri ambao wana nia ya kuajiri wahitimu wenye maadili.

Aliwataka wanafunzi wenzake kuzingatia agizo hilo a kwa sababu inakusudiwa kwa manufaa yao.

“Wenzangu wasichukulie agizo hilo kama adhabu bali ni hatua nzuri kwa manufaa yao, na wale ambao ni lazima wavae mavazi yalioharamishwa wakiwa nje chuo wana uhuru  wa kuchagua cha kuvaa hata kama wanataka kutembea. uchi,” alisema.

Maoni kama hayo yalitolewa na wanafunzi wa kike ambao walisema mavazi ya kichochezi ya wenzao yamekuwa yakichangia visa vya uhalifu wa kingono chuoni humo na kuchangia kukithiri kwa visa vya mauaji ya wanawake nchini hivi maajuzi.

“Kama wanawake tusiwajaribu wanaume kwa kuvaa nguo za kuchukiza. Baadhi ya mavazi haya yamechangia visa vya ubakaji kwa wanafunzi katika chuo hiki na kuchangia kuongezeka kwa visa vya mauaji ya wanawake nchini kwa ujumla,” alisema mmoja wa wanafunzi wa kike.

Chuo kikuu hicho kimetangaza pia kupiga marufuku mavazi kama sketi ndogo, suruali ya kubana ngozi, suruali ya jeans iliyochanika au iliyochanika, blausi za tumbo au shati-tao na blausi au magauni ya chinichini.

Nguo nyingine ambazo zimepigwa marufuku ni pamoja na suruali za kulegea, nguo zinazoonyesha kifua, champati aina ya rocs, kaptula ndogo na nguo za uwazi au nguo zinazoonyesha kamba za sidiria au shati-tao zisizo na mikono na fulana zenye maandishi machafu.

Marufuku hayo si mageni nchini kwani vyuo vikuu vingine tayari vimefanya hivyo.

Miongoni mwa vyuo vikuu ambavyo tayari vimepiga marufuku uvaaji wa mavazi kama hayo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), Kabarak, Chuo Kikuu cha Eldoret, na Masinde Muliro miongoni mwa vyuo vingine.

Jamii zinazoishi karibu na vyuo hivyo zilipongeza hatua hiyo ya kijasiri.