BAMBIKA: Waliondoka bila kakitu?
LEO Ijumaa anazikwa rapa lejendari Chris Kantai, maarufu Chris Kantadda nyumbani kwao Ngong.
Kantadda aliyevuma miaka ya nyuma alifariki yapata wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka 42.
Wasanii wamekuwa wakiendeleza kampeni za kuchangisha fedha kwa ajili ya kuifariji familia yake changa aliyoiacha nyuma ya mke na mtoto mmoja.
Kifo cha Kantai kimeibua maswali mengi huku akifariki akiwa mmoja wa mastaa wa burudani waliotuaga wakiwa hoi kifedha nchini.
Tiririka na listi hii.
Mzee Ojwang
Hata baada ya kuigiza kwa zaidi ya miaka 30 kwenye vipindi maarufu kama Vitimbi, Vioja Mahakamani miongoni mwa vinginevyo, mvunja mbavu Benson Wanjau maarufu Mzee Ojwang alimalizia maisha yake kwa mateso.
Ojwang anayetajwa kuwa mwanzilishi wa komedi nchini, alifariki akiwa na umri wa miaka 78, akiwa hana lile wala hili ila nafsi yake tu.
Shirika la habari la KBC lilishtumiwa kwa kumtumia kwa zaidi ya miongo 30 kisha kumtelekeza.
Akifariki, Mzee Ojwang alikuwa ameajiriwa na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ambapo mshahara wake ulikuwa umepanda hadi kufikia Sh50,000 katika miaka yake ya mwisho.
Licha ya kazi hiyo aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 17, ukiongeza na kipato alichopiga kupitia uigizaji pale KBC, bado Mzee Ojwang aliishi maisha ya kawaida sana.
KBC ilipoamua kumfuta kazi Julai 2014, inasemekana haikumlipa hata senti moja ya kiinua mgongo wake.
Umaskini wake ulikuja kudhihirika alipougua kutokana na umri mkubwa na kushindwa kugharimia matibabu yake kwa ukosefu wa fedha.
Hapo ndipo serikali iliingilia kati baada ya hali yake kuangaziwa na vyombo vya habari.
Alifariki mwaka mmoja baadaye.