Makala

Barabara ya lami huko Lamu yageuka kilio kwa wakazi

Na KALUME KAZUNGU September 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAMII ya wafugaji katika vijiji vya Koreni, Mapenya na Mkunumbi kaunti ya Lamu imelalamikia ongezeko la visa ambapo magari yanayoendeshwa kwa kasi huwaangamiza mifugo wao.

Jamii hiyo sasa imetisha kuifunga barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen kufuatia visa hivyo ambavyo vimekithiri.

Barabara hiyo ilipotiwa lami na kufunguliwa mwaka wa 2021, jamii zinazopakana nayo zilitumai kupokea maendeleo tele ikiwemo nafasi za uwekezaji na biashara, lakini sasa wafugaji wameibua malalamishi wakitaka hatua zichukuliwe.

Kisa cha hivi punde zaidi ni cha Jumapili usiku, ambapo ng’ombe watano waligongwa na lori na kuuawa papo hapo eneo la Koreni, ilhali wengine wakiachwa na majeraha mabaya.

Msemaji wa jamii ya wafugaji Lamu Muhumed Kalmei, alisema magari hayo yanayoendeshwa kwa kasi huwa hayasimamishwi punde yanapogonga mifugo wao.

“Mwendo wa saa moja jioni ya Jumapili, lori lililokuwa limetoka upande wa Mombasa kwenda Lamu liligonga ng’ombe wetu watano na kuwaua. Kuna nyingine kama tatu hivi ambazo ziko hali mahututi. Tumechoka. Ikiwa serikali haitamulika hili, tutaandamana barabarani hivi karibuni na kufunga shughuli zote za uchukuzi,” akasema Bw Kalmei.

Jamii hiyo inasema mara nyingi imejitokeza kuiomba serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Ujenzi wa Barabara Kuu Nchini (KeNHA) kuweka alama za barabarani na matuta kuwezesha madereva kudhibiti mwendo wanapopitia vijiji vyao.

Vijiji vyote vitatu viko pembezoni mwa barabara hiyo.

Juhudi za kupata maoni ya asasi husika za serikali hazikufua dafu kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii.

Bw Sadiq Muktar, mkazi, anaamimi endapo alama za barabarani za kuashiria eneo lao hupitia mifugo kwa wingi zitaekwa, hasara inayowakumba kila wakati ya mifugo wao kugongwa itapungua.

“Karibu kila mwezi tunapoteza ng’ombe 15 kupitia kugongwa na magari eneo hili. Tangu barabara yetu itiwe lami na kufunguliwa rasmi 2021, tumepoteza mifugo wa kima cha karibu Sh4 milioni kupitia kugongwa na magari. Watuwekee hayo matuta kudhibiti hali hii. Tumechoka,” akasema Bw Muktar.

Hivi majuzi, watumiaji wa barabara hiyo pia waliishinikiza serikali kufyeka vichaka pembezoni mwa barabara hiyo kuzuia uwezekano wa magaidi kutekeleza mashambulio.

Miaka ya awali, magaidi wa Al-Shabaab walikuwa na hulka ya kuvamia magari ya usafiri wa umma, yale ya walinda usalama na wasafiri wengine na kuyashambulia kwa risasi na vilipuzi wakiwa wamejificha vichakani.

Mwaka 2018, serikali kuu ilikata vichaka vyote, ambapo kila upande ulifyekwa upana wa mita 50.

Hatua hiyo ilisaidia kupunguza mashambulio ya kigaidi barabarani hadi wa leo, ambapo vichaka vimeongezeka tena.