Baraza la Agikuyu lakataa polisi kwa mikutano yake
NA MWANGI MUIRURI
BARAZA la jamii ya Agikuyu sasa limepuuzilia mbali wito wa kulitaka liwe likiomba ruhusa kutekeleza hafla zake za kitamaduni.
Tangu Desemba 31, 2023, ambapo wakongwe 23 walikamatwa katika Kaunti ya Murang’a wakihusishwa na kundi haramu la Mungiki, kumekuwa na kurushiana cheche za maneno kati ya baraza hilo na Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Wakongwe walioshtakiwa katika mahakama ya Murang’a walivutia wanasiasa wa mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya kuwa watetezi wao.
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Narc-Kenya Martha Karua, kinara wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na wakili Ndegwa Njiru, walifika katika mahakama hiyo kuwatetea wakongwe hao wa umri kati ya miaka 60 na 90.
Waliachiliwa huru mnamo Februari 28, 2024, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutupilia mbali mashtaka yao.
Sasa, baraza hilo likiongozwa na mwenyekiti wake Bw Wachira Kiago lilifanya mkutano Jumamosi katika Mkahawa wa Blue Springs ulioko Kaunti ya Nairobi likikataa kile liliita ‘kukaliwa’.
Bw Kiago alisema kwamba serikali imetoa amri kwamba hafla za kitamaduni za baraza hilo ziwe zikipigwa msasa na polisi.
“Tumeagizwa kwamba tuwe tukitoa ratiba yetu kwa polisi. Eti tuwe tunawahusisha wakuu wa usalama katika kupanga hafla zetu. Hilo ni agizo tunalopinga,” akasema Bw Kiago.
Bw Kiago aliteta kwamba “hata sisi hatushirikishwi katika hafla za polisi”.
“Polisi huwa na utaratibu wao na kwa kuwa hata sisi kama jamii huwa na siri zetu, hatutakubali kuwa na polisi katika vikao vyetu,” akaeleza.
Bw Gachagua akiwa katika Kaunti ya Murang’a mnamo Februari 10, 2024, alikuwa ametangaza kwamba ushirikiano wa baraza hilo na polisi unaweza kusaidia hafla za kitamaduni kutotekwa nyara na wahuni wa Mungiki, kundi ambalo lilipigwa marufuku.
“Tungetaka watu wote hapa Mlima Kenya waelewe kwamba hatutakubali vijana wachache kuharibu mila na utamaduni kupitia kuteka nyara hafla za utamaduni. Ndiyo sababu polisi watahusishwa kikamilifu katika kuandaa hafla za utamaduni,”akasema Bw Gachagua.
Lakini Bw Kiago alisema kwamba “sisi tuko na mikakati yetu ya kutambua wanachama wetu na hatuwezi tukakubali kuwa na wakora miongoni mwetu”.
Alimtaka Bw Gachagua aeleze watu wa jamii za eneo la Mlima Kenya kama jamii nyingine nchini hutolewa amri ya kuandaa hafla zao katika vituo vya polisi.
“Tutahusisha namna gani watu ambao sio wanachama na wengine wakiwa hata sio wa jamii yetu? Bw Gachagua aelewe kwamba hilo tunapinga vikali,” akasema.