Makala

Barobaro ‘mwelewa shida’ ajitokeza kuwafaa wanafunzi, vijana mabandani

April 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

MKENYA anayeishi katika mitaa ya mabanda atakuambia maisha si rahisi hata kidogo.

Hayo ndio maisha ambayo barobaro Anthony Abu anayafahamu tangu utotoni mwake.

Amezaliwa, kulelewa na kusomea katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi.

Hata hivyo, ameanza safari ya kujaribu kubadilisha maisha ya wakazi wa mtaa huo, ulio katika eneobunge la Embakasi Kusini.

“Nimezaliwa na kulelewa katika mazingira ya mtaani, yenye changamoto nyingi sana. Hata hivyo, kuzaliwa katika mazingira haya hakumaanishi kuwa daima wenyeji wataishi kwa hali hizo. Hilo ndilo limenisukuma kuanza juhudi na mikakati ya kuwakomboa wakazi, hasa vijana,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Kwa ushirikiano na mashirika kadhaa ya kijamii, barobaro huyu ameanza mikakati ya kuwakomboa vijana waliozama kwa matumizi ya mihadarati, uhalifu na vitendo vingine visivyolingana na maadili ya kijamii.

Pia, amekuwa akiwasaidia wasichana wadogo waliobalehe kupata sodo, kwani wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kupata bidhaa hiyo muhimu wakati wa hedhi.

“Wasichana wengi katika eneo hili wanatoka katika familia maskini. Wakati mwingine, baadhi ya familia huwa zinakosa hata chakula. Hivyo, kwa baadhi ya wazazi, huwa ni kibarua kigumu kwao kupata pesa za kuwanunulia sodo,” asema kijana Abu.

Anakiri kwamba katika harakati za kutangamana na baadhi ya wasichana, baadhi walimwambia walipata mimba kwa kukosa pesa za kununulia sodo!

“Inasikitisha sana kuwa baadhi ya wasichana wa shule za msingi hapa mtaani wamekuwa wakipata mimba, baada ya kulazimika kushiriki ngono ili kupata pesa za kutumia kununua sodo. Sikitiko ni kuwa, baadhi yao wako katika Gredi za Sita au Gredi ya Saba! Ni hali inayosikitisha sana,” akasema.

Baadhi ya mashirika ambayo amekuwa akishirikiana nayo ili kutoa sodo bila malipo kwa wasichana katika eneo hilo ni Shirika la Dreams, Shofco, Nivalishe Pads na Kagis.

Shirika la Mukuru Justice Centre pia limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika kutetea haki za wakazi wa eneo hilo.

Anasema wasichana walioathiriwa sana na hali hiyo ni wale walio kati ya miaka 10 na 24.

Pia, amekuwa akishirikiana na diwani wa wadi ya Kwa Njenga, Bw Francis Kimondo kuendesha miradi ya kuwasaidia vijana.

Kulingana na Abu, msukumo wake mkuu wa kujitosa katika harakati za kuwakomboa vijana ni “hatua ya viongozi wengi kufumbia macho matatizo na changamoto zinazowakumba vijana wengi”.

“Vijana wetu wanapitia katika hali ngumu. Hata hivyo, ni viongozi wachache sana wanaoelewa matatizo wanayopitia, kwani wengi wao ni wazee. Wengi wao hawana ufahamu kuhusu matatizo ya vijana wa kizazi cha sasa, maarufu kama Generation Z (au Gen Z). Katika hali hiyo, nimeamua kuwa ‘balozi’ na ‘mkombozi’ wa vijana,” akasema.

Anasema viongozi wanafaa kufahamu kuwa kuna miradi mingi ambayo wanaweza kuwasaidia vijana kuiendesha, hasa wale wenye ujuzi kama wa sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT).

Vilevile, anawarai viongozi katika eneo hilo kuwashirikisha vijana  katika masuala kama vile kandanda, kwani “ndio mchezo pekee unaoweza kuiunganisha jamii nzima”.

“Lengo langu ni kuwa mkombozi wa eneo hili kwa hali yoyote nitakayoweza,” akasema.

Aliongeza analenga kufanya hivyo kwa kushirikiana na viongozi waliopo na mashirika yanayoelewa changamoto wanazopitia watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda.