Makala

Biashara ya kuuza mayai ya uzazi ya wanawake yanonga kwa kukosa ajira

Na ESTHER INTABO August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAWAKE wachanga wamegeukia biashara isiyo ya kawaida ambapo wanauza mayai yao ya uzazi kupata hela za kujikimu, kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha na ukosefu wa ajira nchini.

Wanadada hao wanaruhusu madaktari katika kliniki za uzazi kutoa mayai yao kisha yanapewa wanandoa wanaotamani kupata watoto.

Idadi kubwa ya wanawake hao wanashawishiwa kupitia mitandao ya kijamii kwa ahadi ya kunufaika pakubwa kifedha.

Baadhi hurudi mara kadhaa kutolewa mayai zaidi, hali ambayo inahatarisha afya yao.

Mwaka 2022, Loice Mwende alitamani kumwokoa mwanawe aliyekuwa kipofu na kupooza ubongo.

Madaktari walipendekeza upasuaji uliohitaji Sh250,000 ambazo mama huyo, aliyekuwa na umri wa miaka 21 wakati huo, hangemudu.

Loice alikuwa amesikia kuhusu biashara ya kutolewa mayai hapo 2017, lakini wakati huo haikuwa na maana kwake. Hata hivyo, aliposakamwa na matatizo ya kifedha miaka mitano baadaye, aliikumbuka.

“Nilidhani nitaenda kutolewa mayai tu kila mwezi kama kazi ya kawaida hadi nikusanye hela za kutosha,” anatanguliza Loice.Mchakato ulianza kwa kufanyiwa vipimo vya homoni na damu vilivyoonyesha ako shwari kutolewa mayai hayo.

Alikuwa na uzani wa kilo 48.Wiki mbili zilizofuata alidungwa sindano kuwezesha mwili wake kuzalisha mayai zaidi.

“Haikuwa uchungu kamwe. Ilichukua chini ya saa moja,” anasimulia kuhusu utaratibu huo.

Athari pekee zilizojitokeza siku zilizofuata ni uchungu wa hedhi, ila nao uliisha haraka.Alilipwa Sh50,000; kiasi kidogo ikilinganishwa na pesa alizohitaji kwa upasuaji wa mwanawe.

Alirejea mara ya pili na kuelezwa kwamba hana mayai ya kutosha, huku daktari akionya huenda akatatizika kupata watoto siku za usoni.

“Hilo lilinikwaza mno. Wazo kuwa huenda nikashindwa kupata mtoto mwingine liliniboronga kihisia,” akiri.

Vanessa Wanji, 23, anaishi maisha ya kifahari: likizo Diani, hoteli kubwa kubwa Nairobi na mavazi ya mitindo ya kisasa. Lakini ameficha maelfu ya wafuasi na marafiki zake mitandaoni kuhusu anavyogharimia starehe hizo.

“Nilianza kutolewa mayai kwa sababu, kwa kweli, singemudu maisha niliyotaka. Kila aliyenizingira alionekana kuishi maisha ya kifahari, picha wakiwa sehemu maridadi, kuvalia wigi za thamani. Nilitaka hayo pia lakini sikuwa na hela,” asimulia.

Alisikia kwa mara ya kwanza kuhusu kutolewa mayai ya uzazi kupitia rafiki kwenye kundi la WhatsApp, kabla ya kumpa nambari ya kliniki.

Malipo yake ya kwanza Sh80,000 yalimbadilisha maisha.

“Nilinunua simu, mavazi mapya na hata nikaenda likizo Pwani. Kwa mara ya kwanza nilihisi kuwa kiwango sawa na marafiki zangu mitandaoni,” aeleza.

Lakini hadhi hiyo iliandamana na uchungu wa mwili na kihisia.

Stacy Stephens, 26, ametolewa mayai yake mara sita katika kliniki tofauti Nairobi, baadhi ambazo hata hazijasajiliwa. Kwa jumla amepokea takriban Sh500,000.

“Nililipa madeni yangu, nikawasaidia wadogo wangu nahata kuanzisha biashara ndogo mtandaoni. Pesa hizo zilinisaidia kujikimu. Kwa kweli, unapoonja pesa za haraka kama hizo unarudi kila mara,” anakiri.

Hata hivyo, Baraza la Madaktari Nchini (KPMDU) limeelezea wasiwasi kuhusu ongezeko la wasichana wachanga wanaotolewa mayai yao ili wapate hela, pasipo wao kuelewa athari za kiafya.

“Sindano zilikuwa uchungu. Nilifura tumbo, nikapata maumivu ya hedhi, na kuathiri na mabadiliko ya mara kwa mara ya hisia. Lakini pindi hela zilipoingia akaunti yangu, nilijiambia hayo yote yalistahili ili niishi kwa raha. Sidhani hata nilisikiza kwa makini walipofafanua athari za utaratibu huo. Nilitaka tu pesa!” anakiri mwanadada huyo.

“Kila wakati kuna haja ya mayai,” anaeleza Dkt Charles Muteshi, mtaalam wa uzazi katika Hospitali ya Aga Khan.

“Wanawake wanataka kuongeza familia zao, lakini wakati mwingine mayai yao huisha.”

Wanaotolewa mayai ni sharti wawe wamehitimu umri wa miaka 21 na wasipite 35.

“Haturuhusu wanawake wachanga zaidi kwa sababu huenda wakajutia maamuzi yao baadaye. Idadi kubwa ya wanaotolewa mayai ni kati ya miaka 21-35,” anaeleza Dkt Muteshi.