• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Biashara ya mitego ya panya na ‘nyumba za kuku’ yasaidia vijana kukidhi mahitaji yao Nakuru

Biashara ya mitego ya panya na ‘nyumba za kuku’ yasaidia vijana kukidhi mahitaji yao Nakuru

Na PHYLLIS MUSASIA

HALI ya maisha kwa vijana wengi mjini Nakuru, ilikuwa kawaida hadi mapema Aprili janga la ugonjwa wa Covid-19 lilipobadili mambo.

Kwa muda wa kipindi kifupi, athari za kiafya zilienea na kuwazuia watu wengi kubadili jinsi ya kufanya mambo ikiwemo biashara.

Vijana waliotegemea biashara ndogondogo kama vile kuuza matunda na mitumba waliathirika pakubwa na kulazimika kutafuta njia mbadala ya kujikimu maishani.

Anthony Maina, 27, wa eneo la Bondeni, Nakuru Mashariki, hapo awali alichuuza nguo za mitumba katika mitaa mbalimbali ya mji wa Nakuru lakini kwa miezi minne sasa, amekuwa akitengeneza vifaa maalumu vya kutega panya na nyumba za kufugia kuku.

Maina mwenye umri wa miaka  anasema ugumu wa kulipa kodi ya nyumba, kununua chakula na kushughulikia familia yake ulimsukuma kufanya kazi hiyo ambayo sasa ni kitegea uchumi kikubwa kakwe pamoja na vijana wengine wengi.

“Wachuuzi ndio walikuwa watu wa kwanza kufurushwa mjini wakati serikali ya kaunti iliweka mikakati ya kupunguza shughuli za watu mjini ili kuzuia maambukizi. Wakati huo ndipo changamoto ya fedha ilianza kwa sababu ya ugumu wa kuendesha biashara,” akasema.

Maina alisema baada ya steji za magari na masoko kuhamishwa kutoka mjini hadi nje ya mji na kupunguza idadi ya watu, hakuweza kupata pesa zozote licha ya kujikakamua kwa hali na mali.

“Muda uliyoyoma na nikaona ni vyema ikiwa nitawaza tofauti. Majukumu yalianza kunilemea na ikawa wazi kwamba huenda mambo yasirejee kawaida hivi karibuni,” akasema Maina.

Kulingana naye, alijadiliana na rafiki yake John Mungai kuhusu kujiengua kutoka uchuuzi na kujaribu ufundi katika sekta ya juakali.

“Nilikuwa nimeona mzee mmoja katika barabara ya Barnabas akitengeneza mitego ya panya na biashara yake ilionekana kufanya vizuri zaidi. Nilipowaza kuijaribu kazi hiyo, nilikuwa na matumani nitafaulu,” akasema.

Rafiki yake ambaye ni Mungai alikubali kujiunga naye na kwa pamoja wakatafuta jinsi ya kupata mafunzo kabla ya kuanza kazi rasmi.

Wakati wa wiki za kwanza mbili, Maina alisema kulikuwepo na changamoto ya kupata vifaa vya kazi.

“Kubadilisha kazi si jambo rahisi haswa ikiwa ni kazi ya kujiajiri. Unahitaji hela za kuanza kazi hiyo na kwa sababu nilikuwa nimeacha kazi ambayo haikunipa riziki kwa muda, ilikuwa vigumu kwangu,” akasema.

Changamoto nyingine alisema hakuwa na uhakika ikiwa wangepata wateja ambao wangethamini kazi yao.

Baadhi ya watengenezaji wa mitego ya panya na nyumba za kuku eneo la Bondeni, Nakuru. Picha/ Phyllis Musasia

Mara ya kwanza, wawili hao walitengeneza mitengo 30 ya panya bila kuuza yoyote kwa muda lakini waliendelea kujipa moyo.

“Tulijua kwamba mtaa wa Bondeni ulikuwa na soko nzuri kwa biashara yetu na tukawa na subira ili wakazi wawe na nafasi ya kuzoea uwepo wetu sehemu hii,” akasema Maina.

Jinsi muda ulivyosonga, wawili hao walianza kupata wateja na biashara ikanoga huku wakilazimika kutafuta wafanyikazi zaidi.

Wakazi wa maeneo mengine pia walianza kuwatembelea vijana hao na kukunua bidhaa kutoka kwao.

Wazo la kuanza kutengeneza vifaa vya kufuga kuku lilizaliwa kufuatia hamu ya wateja ambao walikuwa wanaulizia kila mara.

“Tuliona ni wazo nzuri na tukafanya bidii kwani tulijua kwamba tutafaidika,” akasema.

Kufikia sasa, Maina na Mungai wanafanya kazi pamoja na vijana wengine wanne na kuongeza idadi yao hadi watu sita.

Mtego mmoja wa panya unazwa kwa Sh200 huku vifaa vya kufuga kuku vikiuzwa kati ya Sh600 na Sh1,200.

Kundi hilo ambalo linaendesha shughuli hiyo kando ya barabara, limeitaka serikali ya kaunti kuwasaidia kujenga sehemu itayowazuia wakati wa jua na mvua.

Vijana hao walisema hawana nia ya kurejelea uchuuzi na maono yao ni kuhakikisha wanapanua biashara hiyo hata zaidi.

You can share this post!

Wizara yapendezwa na jinsi Mombasa inavyokabili Covid-19

Serikali Sudan yatia sahihi mkataba wa maelewano na waasi...