Makala

Biashara zaimarika, mkopo wa Hustler Fund ukiongezwa mara tatu

Na FRIDAH OKACHI December 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIAKA miwili baada ya mradi wa Hustler Fund kuzindulia nchini na Rais William Ruto Novemba 2022, wafanyabiashara mbalimbali wameelezea kunufaika baada ya biashara zao kunawiri.

Mkazi wa Nairobi na mfaidi wa Hustler Fund Lilian Miseva anasema kuwa alikuwa akifanya kazi ya uchuuzi kwenye barabara ya Uhuru Highway, hivi sasa anamiliki duka katikati mwa jiji la Nairobi.

“Mwanzo nilichukua mkopo wa Sh1,000 na kununua vitu kadhaa vya kuuzia wateja wangu. Nililipa baada ya siku 14 kisha nikapata mkopo mwingine,” asimuli Bi Miseva.

Mfanyabiashara huyo asema alizidi kutia bidii hadi kufanikiwa kupata mkopo wa hela nyingi ambao ulimwezesha kufungua duka nje ya jiji la Nairobi.

“Nafurahia sasa hivi sizunguki kwenye barabara ila nimetulia na kazi yangu kwenye duka langu,” aliongeza Bi Miseva.

Mfanyabiashara huyo aliomba Wakenya ambao huchukua mkopo huo, kuhakikisha wanaresjesha kwa wakati ufaao ili kuwanufaisha watu wengine.

Katika maadhimisho ya mwaka wa pili wa Hustler Fund katika Jumba la KICC jijini Nairobi, Rais William Ruto alisema mkopo huo, sasa utatolewa mara tatu ya kiwango cha awali ambacho Wakenya walikuwa wakipokea.

Rais Ruto alisema zaidi ya watu 24 milioni wamechukua pesa hizo, milioni saba ikiwa ni wateja wa mara kwa mara ambao hulipa kwa chini ya siku 14.

“Viwango vya wale wateja ambao ni waaminifu watapata mara tatu na siku za kulipa zikiongezeka kutoka 14 hadi 30. Nafurahia leo kuona kuna wateja milioni saba na hii leo tunaenda kuongeza wateja wengine milioni mbili ambao pia wamekuwa waaminifu,” alisema Rais Ruto.

Hata hivyo, aliomba benki za humu nchini kutoa mikopo kwa wateja hao wa Hustler Fund ikiwa ni njia moja ya kuanzisha mpango wa siku zijazo.

“Naomba benki za hapa nchini pia, zitoe mkopo kwa wateja wetu wa Hustler Fund, tuna wale waaminifu ambao benki zikitaka kuwatambua tutatoa orodha,” alidokeza Rais Ruto.

Kwa upande wake, Waziri wa vyama vya Ushirika Bw Wycliffe Oparanya, aliwaondolea hofu wateja wa Hustler Fund akisema kuwa hakuna yule ambaye ameorodheshwa kwa CRB kwa kushindwa kulipa mkopo huo.

Aliwataka wale ambao hawajaweza kutoa fedha hizo kutoa akisema kuwa atafanya mpango wa kuwatembelea kufahamu sababu ya kukosa kulipa.

“Nikiwa ule upande mwingine sikuwa naona kuwa Hustler Fund ikiwa ya maana yeyote, kwa kuwa Wakenya walikuwa wakipewa mkopo wa Sh100 lakini niko upande huu mwingine na ninafahamu umuhimu wake,” alisema Bw Oparanya.

Tangu kuzinduliwa kwa Hustler Fund Novemba 2022, zaidi ya Sh60.5 bilioni zilisambazwa kwa Wakenya milioni 24.7. Asilimia 79.50 ambayo ni Sh48.1 bilioni zikirejeshwa huku Sh12.1 bilioni zikikosa kurudishwa.

Data ikionyesha kuwa asilimia 52 ya wanaopata mikopo hiyo ni wanaume, asilimia 48 ikiwa ni wanawake. Data hiyo pia ikionyesha asilimia 61 ni vijana, 29.3 ikiwa ni wakopaji wenye umri wa miaka 40-59, asilimia 9.4 ikiwa ni Wakenya wenye umri wa zaidi miaka 60.