Bidhaa za pilipili zamletea tabasamu
JANGA la Covid-19 lilipotua Kenya 2020, Leah Karangi aliingilia kilimo cha pilipili na kuongeza thamani, kama njia ya kujiendeleza kimaisha katika kipindi ambapo sekta nyingi ziliyumbishwa.
Akiwa amejifungua mtoto wake wa pili wakati huo, alihamia kwao Kirinyaga na kuanza kilimo cha pilipili kwenye ekari moja ya shamba la babake.
Alitumia mtaji wa Sh20, 000 kuingilia kilimo, lakini changamoto ya bei duni ya pilipili mbichi sokoni – kilo ikiuziwa Sh100, ilimfanya afikirie njia ya kuongeza thamani kwa kutumia sola (nishati ya jua) kuzikausha.
Safari ya ukaushaji pilipili iling’oa nanga na kampuni aliyoipa jina Fire Chilli, ambayo ilipanuka na kuwa Ginene Ltd baada ya kushirikiana na Joseph Kamata, mwanzilishi wa Nulands Ltd – kampuni ya uuzaji mashamba.

Ushirikiano huo wa mwaka 2023 uliwezesha Leah kupata ardhi kubwa ya kilimo Narok, ambako walianza kilimo kwenye ekari tatu. Wawili hao, Leah akiwa amepata nguvu mpya, waliendeleza ukuzaji wa pilipili.
“Hata hivyo, mafuriko yaliharibu mazao yetu yote – tani 9, ndani ya miezi miwili ya kwanza,” Leah anasema. Licha ya hasara hiyo, hawakukata tamaa. Kama isemavyo, mengine yamekuwa historia.
Akiwa na Digrii ya Maendeleo ya Jamii na Saikolojia ya Watoto, Leah ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Ginene Ltd, ambayo inazalisha bidhaa mbalimbali za pilipili hoho, yaani zile kali zilizounganishwa kwa kutumia mafuta, pilipili zilizopondwapondwa (flakes) na zingine kusagwa, na viungo vya vibanzi – chilli sauce na paste.
Leo hii, kampuni hiyo ina ekari 10 za pilipili Narok na imejumuisha mazao kama komamanga (pomegranate), joka (dragon fruit), papai, karakara, ndimu., na machungwa.

Kituo cha kuchakata bidhaa kiko Karen, Nairobi. Leah anaeleza kwamba vifaa vya jikoni kama vile blenda, sufuria, jiko la gesi na vijiko vinatosha kwa uongezaji thamani bidhaa za pilipili.
“Pilipili hukaushiwa shambani (Narok) kwa nishati ya jua – sola, kisha zinasafirishwa hadi Karen,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano.
Aidha, huchakatwa kuwa flakes au unga. Flakes hutengenezwa kwa kukausha pilipili halafu zinapondwapondwa kuwa vipande vidogo.
Mafuta ya pilipili huzalishwa kwa kuchanganya mafuta ya mboga na viungo kama pilipili manga (black pepper), karafuu, kitunguu saumu, tangawizi, iliki (cardamom), mdalasini, na coriander yaani dhania.
Mafuta hayo huchemshwa pamoja na flakes kwa saa kadhaa kabla ya kusafishwa. Ginene huzalisha lita 100 za mafuta ya pilipili kwa wiki, kiasi sawa na hicho cha sauce na paste.

Flakes na unga huzalisha tani moja kila wiki. “Wateja wetu ni hoteli, mikahawa na watu binafsi Nairobi, Kiambu, Kirinyaga, na Narok,” Leah anadokeza.
Ginene Ltd pia ina kitalu cha kuotesha miche, ambapo mimea michanga ya pilipili hukuzwa kwa wiki sita kabla ya kuhamishiwa shambani, na mazao kuanza kuvunwa baada ya mwezi mmoja.
Leah anaeleza kuwa pilipili ni zao lenye thamani kubwa, na lina changamoto kiduchu za wadudu au magonjwa, na vilevile linaweza kuvunwa kwa miaka mitatu mfululizo baada ya upanzi.
Narok ikiwa ni eneo kame, kampuni yao hutegemea mabwawa kuhifadhi maji ili kuendeleza uzalishaji.
Ginene na Nulands wana wafanyakazi 12 wa kudumu, na huajiri vibarua kazi zinapokuwa kibao hususan msimu wa mavuno na maonyesho ya kilimo na kibiashara.

Changamoto kubwa kwa Leah ni ukosefu wa mtaji wa kutosha, japo mapato yote hurejeshwa kwenye biashara ili kuipanua. Akiwa Meneja wa Uzalishaji wa Ginene Ltd, Leah anaamini kuwa njia ya kipekee kuunda faida kupitia kilimo ni uongezaji thamani.
Ana matumaini kuwa uchakataji wa bidhaa za kilimo utasaidia kupunguza ukosefu wa ajira haswa kwa vijana na kufanikisha ajenda ya maendeleo ya viwanda nchini.
Alipoulizwa ikiwa anaweza kurejea kwenye ajira za ofisi alijibu, “Hiyo ni chapta niliyoweka kufuli. Uwekezaji tuliofanya una mapato ya kuridhisha na biashara tunayofanya ndiyo ofisi yangu.”
