Makala

BIDII YA MCHWA: Makomamanga yamemjenga sasa awafaa wenzake

January 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

BAADA ya kukamilisha elimu ya shule ya msingi, Agnes Changawa, msichana mwenye umri wa miaka 15 kutoka Kaunti ya Kwale, aliingilia kilimo kukimu mahitaji yake na familia.

Anafanya kilimo cha makomamanga (pomegranate).

Aliamua kufanya kilimo cha matunda haya kufuatia gharama chache za kukuza miche yake na faida maradufu inayotokana na matunda hayo.

“Wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunipeleka kwa chuo cha kiufundi kujipatia ujuzi, rasilimali wazazi wangu walionayo ni shamba pekee, sikuwa na mtaji mkubwa wa kuanzisha kilimo cha kuku au kitalu cha mboga hivyo nilitafiti kilimo kinachogharimu pesa kidogo,”akaeleza.

Aidha, alieleza kuwa miti ya mikomamanga huchukua miezi tisa hadi mwaka mmoja kabla kuanza kuzaa matunda.

“Mti huu huchukua muda mfupi kupevuka ukilinganishwa na miti mingine, pia unaweza kupandwa katikati ya mimea mingine kama kunde, pojo na mboga bila ya kuziathiri,” akasema.

Alisema miti hiyo haihitaji maji mengi wala dawa za kukinga na wadudu.

“Ikiwa miche midogo nilikuwa naitilia mbolea ya kinyesi cha kuku na mbuzi tunaofuga,” alieleza.

Mti mmoja wa mkomamanga huweza kuzaa zaidi ya matunda 30, huku tunda moja likiuzwa kati ya Sh150 hadi 500 kulingana na ukubwa wa tunda.

Ndani ya mwaka mmoja mti huweza kuzaa matunda 300.

“Mbali na matunda mimi huuza miche kwa wanaotaka kuanzisha kilimo hiki,” asema.

Changawa anasema hajuti kuingilia kilimo hicho kwani kimemwezesha kubadili maisha ya familia yake.

“Nimefanya ukulima huu kwa miaka mitatu sasa, mapato ninayopata kutoka kwa biashara hii yameniwezesha kumudu mahitaji ya familia yangu, kuweka akiba, kusomesha ndugu zangu na hata kujiunga na chuo cha kushona nguo,” alieleza.

Aliongezea kuwa amejiunga na mafunzo ya ukulima ili kumsaidia kuboresha ukulima wake.

Changamoto kuu katika ukulima huu ni kutafuta soko la kuuza matunda hayo.

“Katika mavuno yangu ya kwanza nilihangaika kutafuta wateja, lakini kwa sasa wateja wananifuata nyumbani na wengine wananitafuta katika mitandao ya kijamii,” alieleza.

Watu wengi hutumia matunda hayo kama dawa ndiposa uhitaji wake uko juu.

“Kuna baadhi ya watu wanaamini sharubati ya matunda haya huweza kutibu ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, saratani mbali mbali, magonjwa ya moyo, kupunguza uzito wa mwili na kadhalika, kufuatia virutubisho vilivyoko katika tunda hilo,” alieleza.

Changawa alisema kwa sasa anauza matunda hayo kwa watu binafsi na maduka ya jumla.

Aidha, alisema ana mipango ya kutafuta kipande cha ardhi na kufanya ukulima wa makomamanga pekee.

“Sasa hivi siwezi kuongeza miche hii kwa sababu hili ni shamba la familia, watu wanategemea kupanda chakula kwa hivyo siwezi kuchukua nafasi kubwa kupanda miti yangu,” alieleza.

Aidha alisema ana ndoto ya kuweza kuuza matunda hayo nchi za nje.

Aliwapa ushauri vijana kuwekeza katika ukulima huu akisema una faida maradufu na pia huchangia katika uchumi wa taifa.

“Kuna vijana wengi wanalia uhaba wa kazi, vijana waache kutegemea kazi za afisini na badala yake wajitupe katika ukulima,” alisema.

Bi Changawa alisema kupitia vyama vijana wanaweza kujiendeleza na hata kufungua viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali.