Makala

Black Junior FC yazidi kujiimarisha mashinani

November 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

BLACK Junior FC ni miongoni mwa klabu zinazoyumbisha timu pinzani katika soka ya mitaani hasa ya kuwania mataji na vilevile mechi za kirafiki.

Kulingana na mkufunzi Cyrus Macharia, changamoto za kifedha ndizo zimekuwa mzigo kwao kwa kukosa kuonja kucheza Ligi ya Kaunti ya Murang’a.

“Tulikosa ligi hii mara kadha hata baada ya kufuzu kutokana na matatizo ya ukosefu wa kifedha yaliyotukabili. Hali hiyo imetufanya kushindwa kunawiri hata licha ya kutafuta usaidizi kutoka kwa wahisani,” anasema Macharia.

Maendeleo na ukuaji wa klabu hutokana na kupanda ngazi kuwania mataji mabalimbali ya ligi ikiwemoligi ya Kaunti, kulingana na kocha huyo.

Anadokeza kuwa viongozi wa klabu yake wamekuwa wakizuru ofisi za Kaunti ya Murang’a ili kutafuta fedha za spoti mbali na kuzuru maeneo mengi kusaka udhamini kutoka kwa washikadau.

Klabu hii kulingana na Macharia inahitaji kuwa na hazina ili kuiwezesha kupiga hatua kubwa kwa kuendesha maswala yake ya soka bila matatizo.

Mazoezi yao hufanyika katika uwanja wa shule ya msingi ya Karumu, Kandara baina ya siku za Jumatatu na Ijumaa.

Nidhamu yadumishwa

Anasema kwa wakati huu ana kikosi cha wachezaji 26 huku wakidumisha nidhamu ya hali ya juu uwanjani.

Kwa vile ari ya kila timu ni kuona inasonga mbele, timu hii imecheza mechi za kujipima nguvu, huku ikijiandaa kujisajili kwa ligi ya kaunti ya Murang’a msimu ujao wa 2020.

Hivi majuzi walicheza mechi za kirafiki na kufanya vyema.

Mechi ya kwanza vijana wa Black Junior waliizima Spurs kwa mabao 2-1.

Mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Kanyiri-ini FC ambapo walitoka sare ya 2-2.

Vijana hao waliichoma Nguthuru FC kwa bao 1-0.

Hata hivyo, Black Junior walipoteza mechi yao dhidi ya Kiranga United FC.

Kocha anahimiza wadau kutafuta njia mbadala ya kuwezesha wachezaji wa mashinani kupata wafadhili wa kugharimia shughuli za michezo.

Anasema yeye kama kocha anajitahidi kuona ya kwamba soka inaleta mshikano baina ya wakazi wote wa wa kijiji cha Muruka na maeneo jirani.

Anasema lengo lake pia ni kuwaunganisha vijana wote kutoka vitongoji tofauti sehemu za Kandara kama Kavuruge, Muruka, na Nguthuru.

Kocha huyo anasema ingawa wanakumbwa na changamoto tele, vijana hawa wamemakinika michezoni.