Makala

Blue Nile FC: Kikosi imara kama simba

March 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KLABU ya Blue Nile FC sasa imepania kujituma mithili ya mchwa huku lengo lao kuu likiwa ni kuwatesa wapinzani wao kwenye kipute cha Aberdare Regional League Kundi C.

Kocha wa timu hiyo Harub Swaleh, anakiri ya kwamba wapigagozi wake hawana jingine ila kujifunga kibwebwe kuwakabili mahasimu wao vilivyo na kubaki kileleni msimu wa Ligi ukikamilika.

“Vijana wangu wamekusudia kufanya kweli kwenye michuano ya mwaka huu wa 2019 kuhakikisha wamenasa tiketi ya kupandishwa ngazi mwakani,” anasema Swaleh.

Kocha Swaleh anasema kutokana na jinsi vijana wake wamejipanga wana uhakika watafanya vizuri kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu.

“Vijana wangu wamekubali kufuata maagizo yangu na ndiyo maana kwa sasa wanaongoza jedwali la Ligi wakiwa na pointi 13.

Anasema tayari wamecheza mechi saba, na kushinda mechi nne mfululizo huku wakitoka sare moja na kupoteza mbili.

Hata  hivyo anasema wameshika alama sawa na JYSA FC ya Juja ambayo pia ina pointi 13.

Klabu ya Maragua Homeboyz inakamata nafasi ya tatu ikiwa na alama 12. Vijana hao wameshinda tatu kutoka sare tatu, bila kupoteza mechi yoyote.

Nafasi ya nne

Timu ya Ruiru Sports inakamata nafasi ya nne baada ya kujitupa dimbani kwa mechi sita. Wameshinda tatu, na kutoka sare mbili huku wakipoteza mechi moja pekee. Timu hiyo inajivunia alama 11.

Vijana wa BTL FC ya Ruiru wanafunga katika tano bora timu hiyo ikiwa imecheza mechi saba na kushinda tatu. Timu hiyo imetoka sare mechi mbili na kushindwa mbili, ikiwa na pointi 11.

Kocha Swaleh anatoa mwito kwa marefarii wawe watu wa kuaminika na majukumu yao.

Anasema mechi yao ya mwisho dhidi ya JYSA FC ya Juja ilikuwa na maswala mengi kwa refarii aliyechezesha.

Anasema kwa sababu ya kuchezea uwanja wa wenyeji wao JYSA refa alifuata hisia za mashabiki, jambo ambalo ni hatari kwa kuendeleza soka.

Kocha huyo anazitaja timu ambazo zimekipatia kikosi chake upinzani wa kweli kama Gatunyu Stars, Rhino FC na Mutomo FC ya Gatundu.

Anakisifu kikosi chake kwa sababu vijana hao hawakosi mazoezi ambayo huanza kati ya Jumanne hadi Ijumaa jioni, na hiyo imefanya kikosi hicho kuwa imara kama simba.