Makala

Boinett alifaulu kwa mengi ila alifeli kumaliza ukatili wa polisi

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet alikamilisha hatamu yake ya miaka minne jana na kuacha afisi hiyo ikiwa na mabadiliko kadha pamoja na changamoto si haba.

Bw Boinnet aliteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi mnamo Disemba mwaka 2014 na kuapishwa rasmi mwezi Machi 11, mwaka 2015.

Kuteuliwa kwake na Rais Uhuru Kenyatta kulijiri baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa kwanza David Kimaiyo.

Ni baada ya kuapishwa kwake na aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga ambapo Bw Boinnet aliapa kuziba mianya yote iliyokuwa imeachwa na Bw Kimaiyo.

Kujiunga kwake na Kitengo cha Huduma za Polisi (NPS) ni baada ya kufanya kazi katika kitengo cha ujasusi ambapo alijiunga mwaka 1998.

Aidha, alikuwa amehudumu kwenye kitengo cha polisi mwaka 1984 ambapo alitumikia kutoka nafasi ya chini na kufikia nafasi ya mkuu wa polisi.

Wakati Bw Boinnet anapoondoka mamlakani atajivunia mabadiliko yaliyopatikana katika uongozi wake.

Sifa ambazo hazitasahaulika miongoni mwa maafisa wake wadogo waliokuwa wakihudumu chini yake ni juhudi za kuona maafisa hao wanapata pesa za kuishi kwenye nyumba za nje mbali na kambi zilizokuwa zimezoeleka awali.

Pia, ni wakati wa kuhudumu kwake ambapo Bw Boinnet alileta pamoja vitengo vya polisi vikiwemo vile vya polisi wa kawaida na wale wa utawala. Vitengo hivi havikuwa vinapatana hapo awali.

Kwa kuleta uwiano huo, Bw Boinnet amehakikisha kuwa makamanda wanaongoza maeneo tofauti kwenye vitengo hivyo tofauti vikiwemo vile vya AP, DCI na polisi wa kawaida.

Ni chini ya uongozi wake pia, ambapo Bw Boinnet alizindua Kitengo cha Doria ya Mipakani (Border Patrol Unit), Kitengo cha Ulinzi wa Majengo ya Serikali (The Critical Infrastructure Police Unit), Kitengo cha Dharura katika huduma za polisi (Rapid Deployment Unit) na kile cha kupambana na wizi wa mifugo (Anti-Stock Theft Unit).

Ni juhudi zake pia ambazo zimeona maafisa sasa wakivalia sare mpya ya polisi ambazo zinaendelea kutambulika na kuzoeleka pole pole.

Vile vile, ni kwenye awamu yake ambayo ameleta mfumo mpya wa uongozi wa polisi ambapo ameweza kuweka wakuu wa polisi kwenye kila wodi. Ni mabadiliko hayo ambayo yameondoa cheo cha OCPD na kuleta vile vya SPC.

Hata hivyo, licha ya mabadiliko hayo yanayoonekana kama ufanisi wakati wa awamu yake, si siri kwamba ni wakati wa uongozi wake ambapo kulikuwa na picha mbaya zaidi ya polisi machoni pa umma.

Changamoto

Baada ya kupambana na changamoto za mashambulio ya kigaidi, ni wakati wake ambapo visa vingi vya mauaji yaliohusishwa na polisi vilitokia.

Miongoni mwa visa vya unyama vinavyoaminika kutekelezwa chini ya uongozi wa Bw Boinnet ni pamoja na kile cha wakili Willy Kimani.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 pia visa vya mauaji ya polisi vilizidi kikiwemo kisa cha mtoto Samantha Pendo.

Vile vile, katika ukanda wa Pwani, visa vya mauaji ya vijana hususan mwaka 2018 vilitokea chini ya uongozi wa Bw Boinnet bila kusahau kupotezwa kwa vijana kwa madai ya kuhusika katika ugaidi.

Matukio ya visa vingi vya kujitoa uhai miongoni mwa polisi pia vilitokea wakati wa Boinnet na haya ni baadhi ya mambo ambayo Inspekta Jenerali atakayemrithi Bw Boinnet atatarajiwa kupambana nayo.

Changamoto ya tishio la ugaidi pia bado linasalia kuwa miongoni mwa mambo ambayo yatapaswa kuangaliwa vilivyo kwani hadi sasa bado kumbukumbu za kuuawa kwa watu 21 katika hoteli ya Dusit D2 na magaidi linasalia miongoni mwa Wakenya.