BONGO LA BIASHARA: Aliacha mahindi na mboga akashika zao analouza Ulaya
WAKAZI wa eneo la Kyumbi, Kaunti ya Machakos hukuza mboga aina ya sukumawiki, mahindi na maharagwe katika mashamba madogo kando mwa nyumba zao.
Na wengine hufuga mbuzi, kondoo na hata ng’ombe wachache wa maziwa.
Hata hivyo, tofauti na wenzake, Bi Lilly Nduku Mwanzia anakuza mmea tofauti kabisa: maua aina ya Arabicum ambayo hutumiwa kupamba afisi kubwa, mikahawa na makazi ya kifahari mijini.
Yeye huuza maua haya jijini Aalsmeer nchini Uholanzi kwenye mnada mkubwa unaojulikana kama Royal FloraHolland.
Mnada huo ni mojawapo wa masoko makubwa ya maua duniani.
Waandishi wa jarida hili walipotembelea shamba la mkulima huyo hivi majuzi, Nduku alikuwa akiwasimamia wafanyakazi wake wakivuna maua haya maridadi kwa kutumia visu maalum kwa kazi hiyo.
“Tuliamua kuendeleza kilimo cha maua aina ya Arabicum baada ya kujaribu mimea mingine katika shamba hilo dogo,” akasema Bi Nduku huku akitembea huku na kule katika shamba hilo akishughulikia uvunaji maua.
Anasema alivutiwa na aina hii ya maua miaka mitatu iliyopita alipomtembelea rafiki yake katika eneo la Kilimambogo karibu na mji wa Thika.
“Baada ya kupendezwa na aina hii ya maua niliomba mbegu (bulbs) chache na nikapanda shambani mwangu. Niligundua kwamba maua haya yanaweza kunawiri katika eneo hili kwa uzuri kabisa. Hapo ndipo niliamua kununua mbegu nyingi na kupanda,” Bi Nduku anasema.
“Tulichuma mapato ya kima cha Sh400,000 (baada ya kuondoa gharama zote) kutoka kwa mavuno ya kwanza. Tunataraji kupata faida maradufu wakati wa mavuno ya pili kwa sababu ubora wake umeimarika,” anasema.
Kuwekeza
Mkulima huyu ana matumaini makubwa kwamba ataweza kurejesha mtaji wa Sh2 milioni alizowekeza katika mradi huo baada ya kipindi cha mwaka mmoja, hatua ambayo anaamini hangepiga kupitia ukuzaji wa mimea mingine.
Maua ya Arabicum hufanya vizuri katika mchanga usio na maji mengi na katika hali anga yenye kiwango kadri cha baridi, kulingana Bw Samuel Karanja ambaye ni mtaalamu wa kilimo cha maua.
Hii ndio maana kilimo hicho ni kitega uchumi kikuu katika maeneo kadha ya Nyeri, Kirinyaga, Nakuru, Thika, Limuru na kando mwa milima ya Abadares ambako wakulima wenye mashamba madogo wamekuwa wakitia kibindoni mamilioni ya fedha kila mwaka kwa kuyauza katika masoko ya ng’ambo.
“Ingawa shamba la maua halipasi kuwekewa maji kila mara, maji hayo yawekwe kwa vipimo kwani maji mengi huweza kuleta madhara kwa kuharibu mizizi yake kando na kusababisha magonjwa yanayosababishwa na bakteria,” anasema Bw Karanja.
Shughuli ya kuvuna maua haya huhitaji wafanyakazi wengi. Baadaye vijiti vyenye maua kupangwa kwa gredi mbalimbali kwa kuondoa vile ambavyo vimeathiriwa na wadudu waharibifu au vilivyonyauka.
Kisha hukatwa kwa saizi sawa na kufungwa kwa mafungu ya vijiti 10 kila moja kabla ya kupakiwa katika katoni kadha tayari kusafirishwa sokoni.
Katika shamba la Nduku, shughuli ya uvunaji huendeshwa siku ambayo maua hayo yameratibiwa kusafirishwa hadi Uholanzi kama hatua ya kudumisha thamani yao yasiharibike kwa kunyauka na kupoteza umbo.
Jumla ya wahudumu 16 walioajiriwa katika shamba hilo kukata jumla ya vijiti 250,000 vya maua hayo kwa muda wa wiki nne au tano.
Kila kijiti huuzwa kwa kati ya Sh10 na Sh27 kwa misingi ya gredi mahsusi.
Ili kufaidi kutokana na soko la kimtaifa, wakulima wa maua ya Arabicum wanashauriwa kuvuna zao hilo kati ya miezi ya Machi na Mei.
Huu ndio msimu ambao hitaji la maua ni juu zaidi katika masoko ya kimataifa. Ni wakati huu ambapo hali ya baridi hushuhudiwa kwa wingi katika mataifa mengi ya bara Uropa.
Wakulima na wafanyabiashara ambao huuza maua ng’ambo sharti waidhinishwe na Baraza la Maua Nchini (Kenya Flower Council-KFC) kwani sharti wathibitishe kwamba wana wanunuzi upande ule mwingine.
Bw Karanja anasema kuwa wale ambao wanalenga masoko ya kimataifa wanapaswa kuhakikisha kuwa mashamba yao yameidhinishwa kusudi maua yao yaafiki viwango hitajika katika masoko hayo.
Maafisa wa Shirika la Kukagua Afya ya Mimea (Kephis) katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) hukagua maua kuthibitisha kuwa yametimiza viwango vya ubora vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa.