BONGO LA BIASHARA: Anajikimu na wenzake 3 kupitia jiko hili la udongo
Na CHARLES ONGADI
JIKO ni chombo cha kupikia na kuna aina mbili, linalotumia umeme ambalo hutumika sana mijini na la makaa linalotumiwa na watu wa kawaida.
Lakini kuna aina ya jiko linalotumia makaa kwa wingi ambalo limewafanya wengi kusaka jiko mbadala kupunguza gharama ya matumizi ya makaa.
Hata hivyo, Wambua Nzikali, 34, aliamua kupiga bongo kusaka suluhisho la tatizo hili na kuunda jiko ambalo lingewapunguzia wananchi wa kawaida gharama.
“Niligundua jinsi ya kuunda jiko ambalo linatumia makaa kidogo na kutoa moto mwingi kwa matumizi ya nyumbani,” asema Wambua wakati wa mahojiano na Akilimali katika karakana yake iliyoko pembezoni mwa barabara ya Karisa Maitha, Shanzu, Kisauni Mombasa.
Ni aina ya jiko linalopendwa na wengi kutokana na uwezo wa kuhifadhi moto kwa muda mrefu na wakati huo huo kutumia kiasi kidogo cha makaa.
Mara baada ya kugundua ni biashara ambayo ingempatia tija, Wambua aliamua kuacha kuuza mboga na matunda katika soko Kongowea na kujitosa mzimamzima katika biashara ya kuunda na kuuza aina hii ya jiko.
Kutokana na biashara yake ya awali alipata mtaji wa kiasi cha Sh1,000 aliotumia kununua malighafi kwa minajili ya kuanzisha biashara hii.
Alianza kwa kuunda jiko 5 kwa siku lakini kadri siku zilivyoyomea ndivyo wateja walivyozidi kuongezeka na kumlazimisha kuunda hadi jiko 50 kwa siku.
Alianza kupata oda kutoka kwa wafanyabiashara kutoka maeneo mbali mbali mkoani Pwani jambo lililompatia motisha ya kuchapa kazi usiku na mchana.
Kulingana na Wambua, anaunda aina hii ya jiko kwa kutumia vipande vya mabati anavyonunua kisha kutengeza umbo zuri la jiko.
Kisha mara baada ya kumaliza kuunda umbo hilo, anatumia udongo uliofinyangwa kwa ustadi mkubwa kuweka makaa yanayozalisha moto mkali unaowaka taratibu.
Wambua anaeleza kwamba anatumia udongo badala ya mabati katika sehemu ya kuweka makaa kutokana na kwamba udongo una uwezo wa kuhifadhi moto kwa muda mrefu.
Wambua anafichulia Akilimali kwamba mwaka jana alilazimika kuajiri vijana zidi kumsaidia katika kuunda zaidi jiko hizi zinazozidi kupendwa na wengi.
“Nimeweza kuwaajiri vijana watatu wanaonisaidia kuunda jiko 50 kwa siku ila idadi hiyo ingali ndogo kulingana na mahitaji ya wateja wangu,” asema.
Jiko moja anauza kwa Sh190 kwa bei ya reja reja wakati kwa wateja wa kununua kwa jumla anawauzia kwa kiasi cha Sh250.
Koroso Otoigo, mkazi wa Shanzu anatuambia kwamba alijaribu mara ya kwanza kununua na kutumia aina hii ya jiko mwanzoni mwa mwaka jana na kwa sasa anafurahia uamuzi alioufanya.
“Ni jiko ambalo linahifadhi moto kwa muda mrefu na tena linatumia makaa kidogo ikilinganishwa na jiko la kawaida ambalo limeudwa kwa kutumia mabati,” asema Otoigo.
Ni maoni yanayoungwa mkono na Kadzo Charo anayeuza mahamri na vitobosha katika kituo cha biashara cha Bushbar, Shanzu anayesema kwamba aina hiyo ya jiko linahifadhi moto kwa muda na tena halitumii makaa mengi.
Anasema ni jiko zuri kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia jiko kuundia mahamri, chapati na hata mbaazi kwa kuwa hawatumii makaa mengi.
Kulingana na Wambua ni kwamba kati ya wateja wake ni wafanyabiashara wanaonunua kisha kuchuuza mitaani ama katika soko kuu la Kongowea.
Hata hivyo, Wambua asema kwamba kati ya changamoto anazokumbana nazo katika biashara hii ni wakati mteja anapompatia oda ya kuunda jiko nyingi ila tu kukosa kulipia wala kuyachukua ama wakati mwingine kulipa nusu nusu.
Aidha, anasema kwamba kwa sasa yuko katika mchakato wa kupanua zaidi biashara yake kwa kuongeza kiwango anachounda kwa siku. Hii ni kutokana na wateja kuzidi kuongezeka kila uchao.
Anakiri kazi hii ya kuunda jiko imeweza kubadilisha maisha yake ikimwezesha kulea vyema familia yake mbali na kujenga nyumba nzuri kwao mashambani.
Anawashauri vijana hasa walio mijini kutochagua kazi na kuwa wabunifu kila mara ili kwenda na wakati. Asema kwamba amejitolea kumfundisha kijana yeyote atakayejitokeza jinsi ya kuunda jiko hizi bila malipo.
“Nina vijana wawili waliomaliza masomo ya upili mwaka jana ninaowafundisha kazi hii na karibuni watakuwa wamefuzu na kuanza maisha yao kwingineko,” asema Wambua.