Makala

BONGO LA BIASHARA: Hutia mfukoni kibunda kwa kufuga mbwa wakali

July 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

VIJANA wana mchango mkubwa katika kuimarika kwa uchumi na maendeleo ya nchi kwa jumla.

Hapa nchini Kenya, asilimia zaidi ya 70 ya raia ni vijana.

Hata hivyo, asilimia kubwa ya vijana hawa hawafaidi kutokana na hizi pesa na hawana kazi.

Aidha, serikali huwa inatenga pesa za vijana kila mwaka lakini maisha ya vijana hawa hayajabadilika pakubwa.

Mjini Kenol katika Kaunti ya Murang’a tunakutana na Martin Mwai, 32, ambaye ana dhana tofauti sana na ilivyo kawaida ya vijana wengi ya kutegemea serikali.

Yeye anajihusisha na kazi ya kuwafuga mbwa wa aina mbalimbali wa kuuza.

Bw Mwai alipoanza mradi huu mwaka wa 2015, kilichomchochea ni ari ya miaka mingi ya kuwafuga mbwa wakali.

Hii ilimjia baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili mnamo 2006 na kujiunga na chuo cha kiufundi cha Nairobi.

Mwanzo alinunua mbwa wawili wachanga wa aina ya German Shepherd katika eneo la Nanyuki.

Mbwa hawa wawili; wa kike na wa kiume walimgharimu kima cha Sh35,000 kwa pamoja.

Kulingana naye, aina hii ya mbwa wana uwezo wa kuzaa watoto kati ya saba na wanane baada ya kipindi cha miezi mitano ya ufugaji bora. Kwa kawaida, huwa anawauza wakiwa bado na umri wa kati ya miezi miwili na mitatu kwa bei isiyopungua Sh40,000 kila mmoja.

Martin Mwai akiwa na mbwa wake aina ya German Shepherd katika mji wa Kenol, Murang’a. Picha/ Chris Adungo

Baadaye alipofanya mauzo ya mbwa kwa mara ya kwanza alinunua aina nyingine ya mbwa wanaojulikana kama Rottwailer katika eneo la Nanyuki.

Mbwa hawa wawili walimgharimu jumla ya Sh90,000.

Aina hii huanza kuzaa baada ya kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitano hivi.

Anaelezea ya kuwa Rottwailer kwa kawaida huwa anazaa kati ya vijibwa sita na vinane na kisha baadaye kuwauza kwa bei isiyopungua Sh45,000 kila mmoja mwenye umri wa miaka mitatu.

Bw Mwai pia ana aina nyingine ya mbwa wanaojulikana kama South African Boel aliowanunua mjini Nakuru kwa Sh80,000 kila mmoja, japo kwa kawaida wale wa kike hugharimu hata zaidi ya Sh95,000.

Anapowapa mafunzo na kuwafunga kwa muda wa miezi mitatu, huwa anawauza baadaye kwa kati ya Sh155,000 na Sh157,000. Bw Mwai anaeleza kuwa mbwa wake wote kwa jumla huwa anawapikia wali kiasi cha kilo tano na nyama ya ng’ombe, kondoo au mbuzi kilo nne kila siku. Asipopata nyama, basi mabaki ya chakula na mifupa kutoka nyingi za mahoteli mjini Kenol humfaidi pakubwa.

Pia huwa anawafanyisha mazoezi ya kila siku mmoja baada ya mwingine kwa kuwazungusha mjini Kenol ambayo pia ni njia ya kutoa matangazo kwa wananchi ya kuwa ana mbwa wakali na wajuzi zaidi wa kuuza.

Awapa mbwa mafunzo

Halikadhalika, Bw Mwai huwa anawapa mafunzo mbalimbali kwa kuwazungumzia kwa maneno na kupitia kwa ishara. Kulingana naye, soko la mbwa hawa ni kwa njia ya mtandao ambako huwa anapata wateja wengi kwa namna hii.

Huwa anawapiga picha mbwa wake na kupakia picha hizo kwenye mitandao ya kijamii ambako wanunuzi hupata maelezo zaidi na kuzungumzia namna watakavyowanunua na kwa bei gani.

Mbali na wanunuzi kupitia mtandaoni, kuna wale ambao wanamjua binafsi na wale ambao humjua kupitia kwa marafiki na pia kuwa wateja wake waaminifu vilevile.

Kwa sasa ameagiza aina nyingine ya mbwa kutoka nchi ya Romania anayejulikana kama Caucasian ama Russian Montain Dog na itamgharimu zaidi ya Sh350,000 atakapowasili humu nchini.

Mbwa huyu ana makali ya hali ya juu na watoto wake atakapofikia wakati wa kuuza atakuwa anawauza kila mmoja kwa zaidi ya Sh200,000.

Kazi hii anasema kwake ina faida kuu na ndiyo ajira yake hasa ambayo inamwezesha kupata riziki ya kumtunza mkewe na kukimu mahitaji yote ya kimsingi ya mtoto wao mmoja.

Katika siku za usoni Bw Mwai anatarajia kuanzisha kampuni ya usalama itakayohusika na majibwa na vilevile anatarajia kwamba atapata ardhi kubwa zaidi ya aliyonayo kwa sasa ili kupanua zaidi ufugaji wake wa mbwa na pia kumwezesha kujumuisha mbwa wa spishi au aina mbalimbali.

Pia anatarajia kwamba katika siku zijazo, ataweza kupanua zaidi soko lake la majibwa na kuwafikia wateja kutoka nchi nyinginezo za kigeni kama vile Uganda na Tanzania.