BONGO LA BIASHARA: Kundi la walemavu labuni sodo za kuauni wenye kipato cha chini
Na CHARLES ONGADI
SODO ni kitambaa kitumiwacho na wanawake kujihifadhi wakati wa hedhi.
Aghalabu kila mwezi wao hulazimika kutumia kitambaa hiki kujisitiri.
Hali ya uchochole miongoni mwa baadhi ya jamii nchini imetatiza masomo ya mtoto wa kike kutokana na kutoweza kugharimia sodo.
Katika baadhi ya maeneo nchini wasichana waliobaleghe hukosa ama kuwacha shule kwa kukosa sodo za kujihifadhi wakati wao wa hedhi.
Wakati baadhi uamua kutumia mchanga, blanketi zilizochanika na hata matawi ya miti kujihifadhi wanapokuwa katika hali hiyo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya afya ya kinamama, kila baada ya masaa manne, mwanamke huhitajika kubadilisha sodo kwa manufaa yake ya kiafya.
Ni gharama kwa binti asiye na uwezo wa kununua sodo kila mwezi, jambo ambalo hulazimisha baadhi kuamua kuacha masomo yao ama kutafuta wapenzi kuwapa hela za kununua bidhaa hii.
Hata hivyo, kundi la akina mama walemavu la Tunaweza Women Group, lililoko mtaa wa VOK, Kaunti-ndogo ya Nyali, Mombasa, limeweza kuvumbua aina ya sodo inayoweza kutumiwa kwa kipindi kirefu.
“Baada ya kutambua tatizo sugu linalomkosesha usingizi mtoto wa kike mara anapobaleghe, tuliamua kupiga bongo kutafuta jinsi ya kumaliza tatizo hili,” asema Bi Lucy Chesse ambaye ni mwenyekiti wa kundi hili wakati wa mahojiano na AkiliMali.
Kulingana na Bi Chessi, kundi hilo lilianza kwa kutumia vipande vya blanketi maalum kuunda aina hii ya sodo kabla ya kuvumbua kitambaa aina ya flannel.
Wanashona kitambaa aina ya flannel kilicho na uwezo wa kunyonya uchafu wote na kuiambatanisha na mshono maridadi wenye umbo la mshale.
Huchukua kundi hili lenye wanachama 15 siku tatu kushona sodo 200.
Pakiti moja ya sodo hii ina padi nane zinazoundwa kwa aina mbili ya nguo iliyoshonwa, yenye umbo la mshale, sabuni, taulo, suruali mbili na mfuko maalum wa plastiki.
Ni pakiti maridadi ambayo inaweza kubebwa na mtoto wa kike bila kuona haya kwa sababu inapendeza wala hakuna anayeweza kuelewa kwa haraka kwamba ni sodo.
Bi Chesse anasema kwamba mara baada ya kutumika, mtumiaji anaweza kuosha padi hiyo na kuanika juani ili kuweza kuitumia tena punde inapokauka.
Ama anapokuwa shuleni anaweza kubadilisha bila wasiwasi wowote na kuhifadhi iliyotumika katika mfuko wa plastiki ili kuiosha anaporudi nyumbani.
Bi Chessi anaongeza kwamba pakiti moja wanauza kwa Sh800 wakati padi yenye mishale miwili wakiuza kwa Sh90.
Aidha, Bi Chessi anatuarifu kwamba wamekuwa wakigawa bure bilashi zaidi ya sodo 1,000 kwa shule za msingi na upili katika Kaunti ya Mombasa na hata maeneo ya Samburu .
Kati ya shule ambazo zimenufaika kwa sodo hizi ni shule ya Pwani School for Mentally Challenged, Rising Stars, Olive Rehabilitation School, Victory Academy (Kisimani), North Gate School miongoni mwa nyingine.
Kundi hili la Tunaweza kwa sasa lina oda ya kuunda sodo 200 kwa mfanyabiashara mmoja kutoka nchini Tanzania.
Akizungumza na mwandishi huyu, Bi Petronila Kadzo Katana mkazi wa Mla Leo, Kisauni na ambaye ni mama wa wasichana wawili, anawavulia kofia akina mama hao kwa uvumbuzi wao ambao utawaokoa watoto wa kike kukosa kufika shuleni wakati wao wa hedhi.
“Ni aina ya sodo ambayo ni salama na ni rahisi kubeba mbali na kwamba inaweza kutumiwa kwa muda mrefu,” asema Bi Katana.
Anaongeza kwamba mara ya kwanza kutumia sodo hizo zilimvutia hata kumpelekea kuwanunulia wanawe wa kike.
Si mara ya kwanza kwa kundi hili kufanya uvumbuzi wa nguvu, mwaka jana walivumbua aina ya siagi inayoundwa kwa kutumia njugu.
Kutokana na uvumbi wao, kundi la Tunaweza limepata mwaliko kuonesha bidhaa zao katika maonyesho ya kilimo ya Mombasa mwaka 2019.