BONGO LA BIASHARA: Kusafisha na kupaka viatu rangi humpa riziki kila siku
Na PHYLLIS MUSASIA
KILA asubuhi na mapema Bi Maureen Kimeli hurauka ili kufika katika sehemu yake ya kazi kwa wakati.
Yeye huripoti kwenye duka lake lililoko katika barabara ya Kenyatta mjini Nakuru, mwendo wa saa kumi na mbili na nusu asubuhi ili kushughulikia wateja ambao wanapaswa kufika kazini kuanzia mwendo wa saa mbili hivi.
Kazi yake huwa ni kusafisha viatu vya wateja na kupaka rangi. Kazi ambayo ameifanya kwa muda wa mwaka mmoja sasa.
Maureen ana umri wa miaka 30 na licha ya kusomea kozi ya masuala ya usafiri na utalii, anaazimia kwamba miaka kadhaa ijayo atakuwa na duka kubwa la kuwahudumia wateja ambao wanataka vyatu vyao visavishwe na kung’aa wakati wote.
Kwa siku moja, yeye huhudumia wateja zaidi ya 25 ambapo kila mmoja hulipa ada ya Sh40.
“Ninapoingia hapa mwendo wa saa kumi na mbili na nusu asubuhi, mimi hufanya kazi hadi saa kumi na mbili na nusu jioni wakati ambao huwa nafunga na kurudi nyumbani,” akasema Bi Maureen kwa ujasiri.
Kazi ya kupaka viatu rangi ilisemekana kufanywa na wanaume siku za hapo awali lakini wakati huu, Maureen anasema ameweza kuwashawishi wateja wengi kwa kuifanya kazi hiyo bora zaidi, kuliko hata wanaume wengi ambao hufanya kazi sawia karibu na duka lake.
“Baada ya kuifanya kazi hii kwa muda wa kiasi cha haja, kunao wale wateja ambao hawaendi kwingineko ila hapa tu. Hata wakati ninapochelewa kufungua duka hili, wao hunipigia simu kutaka kujua niliko,” akasema Maureen.
Japo anasema alipitia changamoto wakati wa mwanzo, wakati huu ameizoea kazi yake na kwamba hana tamaa tena ya kutafuta kazi nyingine.
“Mara ya kwanza nilipoanza kazi hii, wateja wengi hawakuamini ikiwa ningeweza kuifanya vyema. Ilinichukua muda mrefu kuwashawishi kwamba ningesafisha viatu vyao na kuving’arisha kwa rangi spesheli,” akasema.
Wakati mmoja alisema alilazimika kufunga duka lake muda wa jioni baada ya kuwahudumia wateja watatu pekee.
Hata hivyo, muda ulipozidi kusonga, alijifunza kuzungumza vyema na wateja wake na hata kuwapa magazeti wasome wakati anapoendelea kuwahudumia.
Mara kwa mara alisema yeye huakikisha kwamba anayo aina tofauti ya magazeti kwa wateja wake.
Maureen hununua magazeti ya ‘Daily Nation’ na ‘Taifa Leo’ ili kuwashawishi hata zaidi wateja wake wanaopenda lugha ya Kiswahili.
“Nilikaa na kuwaza ni mbinu gani ambayo ningetumia kupata wateja bila ya kuwaeleza tu kwa mdomo kwamba ninaweza kuifanya kazi hii hata vyema zaidi. Niligundua kwamba wanaume wengi wanapenda siasa na kwa hivyo njia mojawapo ya kuwavuta katika duka langu ni kuhakikisha kuwa wanapata magazeti yote kila asubuhi na kuchambua siasa wakati mimi niapoendelea kuwang’arishia viatu vyao,” akaongeza.
Maureen anapopokea mteja, mara moja humkaribisha na kumuuliza atasoma gazeti lipi. Baadaye, yeye huanza kazi kwa kusafisha viatu kwa maji, kisha anavipanguza vyema na kuvipaka rangi hadi vinapoonyesha sura ya kung’aa.
“Wateja ambao huja hapa watakwambia wao huchukua muda mfupi sana humu. Jukumu langu ni kufanya kazi ya kuridhisha bila kumpotezea mteja wakati wake,” akasema.
Kwa sababu ya idadi kubwa ya wateja ambao huzuru duka la Maureen, anaye mfanyakazi msaidizi ambaye hushirikiana naye.
Kila siku, Maureen humlipa mfanyakazi wake Sh400 na wakati kazi haijaenda vyema, yeye humpa kati ya Sh250 na 300.
Maureen ni mama wa mtoto mmoja ambaye anasoma kupitia kazi anayoifanya ya kupaka viatu rangi.
Aidha, analipa kodi ya nyumba bila wasiwasi wowote na hata kuwekeza baadhi ya pesa anazopata kila siku.
Kulingana naye, alianza kazi hiyo kwa Sh5, 000 pesa alizotumia kulipa kodi ya duka, kununua viti kadha vya wateja na vifaa vya kazi kama vile rangi, brashi, mtungi wa maji na vitambaa vya kupanguza vyatu vya wateja.
Kila mwezi, Maureen hupata faida ya kati ya Sh15, 000 na Sh20, 000 baada ya kumlipa msaidizi wake na kununua vifaa vya kazi.
Baada ya kukamilisha kozi ya usafiri na utalii katika chuo cha Nairobi Aviation miaka 6 iliopita, Maureen alitarajia kuajiriwa kazi katika baadhi ya kampuni kubwa za kitalii humu nchini.
Lakini licha ya bidii masomoni na ndoto za kupata kazi ambayo ingempa riziki nono ya kila siku, ndoto ya Maureen haikutimia jinsi alivyotarajia.
Hata hivyo, amewahi kufanya kazi katika kituo cha kibinafsi cha mapumziko-Kivu mjini Nakuru, hoteli za Kathy na Grand Winstone zote za Nakuru lakini mapato yalikuwa duni.
“Nilikuwa na wakati mgumu wa kujimudu kimaisha na mara kwa mara nilifungiwa nyumba kwa kukosa kulipa kodi kwa wakati,” akaeleza.
Wakati biashara inaponoga, Maureen hupokea kati ya wateja 25 na 30 kwa siku moja.