Makala

BONGO LA BIASHARA: Mawakala humsaka kwa jinsi anavyofahamu soko la pilipili

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA soko kuu la Kongowea jijini Mombasa, kuna shughuli chungu nzima za uuzaji na ununuzi wa bidhaa za kilimo.

Nicodemus Wali ni mmoja wa wanabiashara mahiri katika soko hili la Kongowea.

Mfanyabiashara huyu huwa anauza aina mbalimbali za pilipili ikiwemo ‘Red Chilly’, ‘Long Chilly’ na ‘Bullet Chilly’.

Wali alianza kazi hii baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili mnamo 2012 katika Kaunti ya Kitui.

Bwana huyu ambaye ana umri wa miaka 28 kwa sasa, huwa anapata mazao haya kutoka mashambani akiwa jijini Mombasa na huagiza bidhaa zenyewe kutoka kwa wakulima wanaohiari kuzisafirisha wenyewe hadi Kongowea sokoni.

Wakati mwingine, wafanyabiashara wa kati (mawakala) hununua mazao haya shambani kisha kumletea sokoni ambapo kwa kawaida huwa ananunua kwa vipimo vya kilo.

Bidhaa zinapofika sokoni, huwa anafanya malipo yake kwa wakulima alionunua kutoka kwao.

Kulingana naye, pilipili aina za Long Chilly na Red Chilly huwa zinapatikana kwa wingi katika eneo la Taveta huku Bullet Chilly ikipatikana sana katika sehemu za Kibwezi.

Long Chilly pamoja na Bullet Chilly kwa kawaida huwa zinachukua muda wa hadi miezi mitatu kukomaa zikiwa shambani huku Red Chilly zikikomaa baada ya kipindi cha hadi miezi minne.

Kila siku ya wiki kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, yeye hufika sokoni saa kumi asubuhi na kurejea nyumbani saa kumi na mbili jioni. Majira ya asubuhi huwa ndio wakati mwafaka wa kupokea bidhaa hizi kutoka kwa mawakala au wakulima wanaozisafirisha hadi jijini Mombasa.

Wali anasema kuwa pilipili aina ya Bullet Chilly huwaniwa sana na wateja na hivyo mara nyingi ana uwezo wa kuuza vipimo vya hadi kilo 500 kwa siku nzuri.

Aina ya Long Chilly kiasi cha kilo 300 humchukua siku kama tatu hivi na Red Chilly kwa upande mwingine huwa inamchukua siku tatu hivi kuuza kiasi cha kilo 100.

“Pilipili kama chakula kingine chochote, zinaweza kuharibika. Kwa mfano, Bullet Chilly inaweza kuharibika baada ya siku mbili huku Long Chilly na Red Chilly zikiharibika baada ya kipindi cha wiki mbili hivi,” Bw Wali anaeleza.

Katika soko hili, Wali anasema kuwa wanunuzi wengi ni wenyeji wa Mombasa, na aghalabu wengi wao ni Wahindi. Kulingana naye, wanunuzi wengine pia wa bidhaa zake huwa ni wafanyabiashara wadogo wadogo na hata wengine ni wafanyabiashara wa kuuza nje ya nchi kwa mfano nchi ya Uganda na Burundi.

Pilipili hizi huwa anazinunua kwa kati ya Sh60 na Sh80 kutoka shambani na kisha kuziuza sokoni kwa hadi Sh100 au Sh120 kutegemea muda na kiwango cha bidhaa sokoni.

Kwa kuwa yeye huuza hadi kilo 500 kwa siku, ina maana kwamba ana uwezo wa kujiundia hadi Sh50,000 au Sh60,000 kwa siku.

Baadhi ya changamoto ambazo huwa anakumbana nazo ni kuharibika kwa zao hili linaponyeshewa likiwa njiani ama sokoni.

Anasema kuwa pilipili zinapopata maji kwa kunyeshewa, huwa zinaanza kuoza baada ya muda mfupi ambayo huwa ni hasara kubwa kwa muuzaji yeyote.

Tena katika misimu ya mvua, baadhi ya maeneo ambayo huwa anapata bidhaa hizi huathiriwa na uharibikaji wa barabara na hivyo basi kuzua changamoto za usafirishaji wa pilipili kutoka mashambani hadi sokoni.

Anadokeza ya kuwa kati ya mwezi wa nne na wa sita, mazao ya pilipili huwa mengi sokoni ambapo huwa inachangia kushuka kwa bei ya bidhaa hizi. Hata hivyo, kuanzia mwezi wa nane hadi wa Januari, mazao huwa yanapunguka na kuongezeka bei.

Anasimulia kuwa kazi hii inamfaa pakubwa kwani ndiyo kazi anayoitegemea kupata riziki ili kuyakimu mahitaji yake binafsi pamoja na ya mkewe na mtoto mmoja.

Aidha, ana jambo moja ambalo anashukuru serikali kuhusiana nalo: ujenzi wa soko hili upya maanake usalama wa bidhaa zao na wao wenyewe umeimarika pakubwa.