BONGO LA BIASHARA: Mila kali zilisukuma kina mama Turkana ‘wajipange’
Na SAMMY LUTTA
KWA jamii ya wafugaji ya Waturkana, mwanamke haruhusiwi kuchinja mbuzi, kondoo au ng’ombe anapohisi njaa.
Aidha, haruhusiwi kuuza mifugo hao bila ruhusu ya mumewe au mwanamume mkuu katika familia hiyo.
Hiki ni kinaya kikuu kwa kuwa jamii hii tangu jadi inajulikana kuwa wakazi wengi wanamiliki mamia ya mifugo na wanawake wametwikwa majukumu ya kuhakikisha kuwa mifugo hao wanapata maji hata kutoka kwa mashimo marefu kwa maeneo yasiyo na mifereji au mito.
Hali hii ilisababisha Arukudi Arupe, 31, mkazi wa kijiji cha Morung’ole katika Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi kuanza kufuga kuku mwaka wa 2017 baada ya kutembelea rafiki yake mjini Kakuma, kilomita 20 kutoka kwake na kujua faida yake.
“Nikiwa kwa rafiki yangu nilipata habari kuwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linatoa mafunzo ya jinsi ya kufuga kuku na baadaye kugawia watu kuku wa kienyeji,” alikumbuka.
Alikuwa miongoni mwa wakazi 200 eneo hilo ambao walipewa kuku 2,000 ili wafuge.
Alieleza kuwa alipewa kuku saba kwenye mradi huo kwa vile hakuwa na uzoefu wa kufuga kuku.
Alitengeneza nyumba ya kuku kando na manyatta yake na baada ya miezi mitatu akaanza kupata faida ya mayai na nyama.
“Kuku ni zangu sasa. Nikitaka nachinja ili watoto wangu sita wapate chakula kitamu. Mayai pia nawapikia na ni rahisi mgeni kuona tofauti ya watoto wangu ukilinganisha na wa jirani,” alisema huku akitabasamu.
Kuku walipoongezeka, Arupe alianza kupata hasara kutokana na nyoka na wanyama wengine wa msitu ambao walikuwa wanavamia kuku wake nyakati za usiku na wakitembea nje kutafuta chakula.
“Kwa sababu ya bidii yangu nilipata ufadhili wa kujenga chumba cha kisasa cha kuku ambacho sasa kimeinuka. Mayai yangu yote, vifaranga na kuku wangu sasa hawaliwi na wanyama wa msituni,” alisema baada ya kuhakikisha kuku wake wote 23 wameingia kwa chumba hicho kabla ya kufunga.
Alisema idadi ya kuku inaongezeka polepole kwa sababu yeye hupenda kuhakikisha kuwa familia yake ambayo iko eneo linalokumbwa na baa la njaa kila wakati wamepata chakula cha kutosha.
Huwa anachinja kuku ili watoto wapate chakula na pia kuuza mjini Kakuma ili apate pesa za kununua chakula kingine kama mahindi, maharagwe, mboga na matunda.
Anauza kuku kuanzia Sh700 hadi Sh2,000 kulingana na uzito wake. Yai moja ni Sh15 na kwa sasa analenga kuwa mfugaji wa kuku bora Kaunti ya Turkana na kuku zaidi ya 1,000.
Arupe sasa anatoa changamoto kwa akina mama katika Kaunti hiyo kujihusisha na ufugaji wa kuku ili kupata faida ya nyama, mayai na mapato wanapouzwa.
Kwa sasa ameanzisha kikundi kiitwacho Morungole Poultry Women Group ambacho wanachama wake wanatoka katika kijiji hicho na wanajihusisha na ufugaji wa kuku. Kila wakati wanachama wanapokutana huelimishana njia mwafaka za kuboresha mradi huo.
Mita 50 kutoka kwa Arupe ni Cymprose Ekadeli ambaye kuku wake sita wanataga mayai na tayari anatarajiwa kupeleka kreti moja ya mayai ya kienyeji kwa hoteli moja mjini Kakuma atakayopata Sh480.
Mumewe Arupe, Aruan Edoket alihoji kuwa kwa miaka mingi alijua kuku kama ndege asiye na faida kama ndege wengine ulimwenguni.
“Mimi kama mwanaume Mturkana nimeishi nikijua kuwa nyama ya kuku ni kidogo sana ukilinganisha na mbuzi. Hii inafanya ufugaji wa kuku kuwa wa hasara sana lakini sasa nimeamini kuwa mwanaume akiruhusu mke kufuga kuku kuna manufaa ya chakula na pesa kama ninavyoshuhudia,” Aruan alisema.
Aliongezea kuwa mbuzi anapochinjwa kuna sehemu nyingi ambazo wanawake hawastahili kula kulingana na utamaduni wa Waturkana na kwa hivyo “kuku imewapatia akina mama afueni” kwa vile wanaruhusiwa kula chochote watakacho.
Mradi huo wa kuku ambao unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya unalenga kushirikiana na Serikali ya Kaunti ya Turkana wa kuhakikisha wakazi wanapata chakula cha kuwapa lishe bora na pia kuuza kupata mapato.
Afisa wa FAO Kaunti ya Turkana David Irura alisema kuwa shirika hilo lilianza na kuku wachache kwa wakazi ambao walipokea mafunzo ya kufuga kuku kwa sababu wengi ni mara yao ya kwanza kufuga kuku.
“Uzuri wa kuku tuliopatiana ni kwamba wanataga mayai mengi, wananenepa haraka na wanatakikana sana kwenye soko. Kakuma iko na soko kubwa la kuku kwa sababu kuna wakimbizi ambao wanaishi eneo hilo na pia wangependa kula kuku,” Irura alisema.
Mradi huo umewawesha akina mama kama Ekadeli kununua nguo zake na za watoto na pia kuwa na pesa za kutafuta matibabu.