BONGO LA BIASHARA: Mshonaji viatu vipya vya shule aliye na soko tayari
Na HASSAN POJJO
KUKOSA kwenda katika shule ya upili baada ya kukamilisha elimu yake ya Darasa la Nane hakukumzuia kupiga hatua katika hali ya kusaka maisha ya kila siku na sasa anapata riziki yake kwa kushona viatu Pwani.
Daniel Mutua, mzaliwa wa Kaunti ya Kitui katika kijiji cha Mbitini, mwenye zaidi ya miaka 45 alishindwa kuendelea na elimu ya Shule ya Upili kwa sababu ya shida za kifamilia.
Alikamilisha elimu yake ya msingi mwaka 1987 na baadaye akafululiza hadi mkoa wa pwani eneo la Changamwe alikoanza kazi ya upigaji picha mtaani.
Alifanya upigaji picha kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya kubadilisha mawazo na kuanza kazi ya ushonaji viatu, kazi aliyokuwa akifanya akiwa shule kwa ajili ya kutafuta riziki alipokuwa kijijini Mbitini.
“Ni kutokana na hali ya maisha ilivyokuwa ndiposa nilianza kujituma tangu nikiwa katika shule ya msingi ili kuona kwamba naweza kujitatulia matataizo yangu binafsi badala ya kutegemea wazazi,” asema Daniel.
Ilipofika mwaka 2001, Daniel alianza rasmi kazi ya ushonaji viatu vipya katika eneo la Chaani muhususi kwa ajili ya watoto wa shule.
Alipendelea kufanya kazi hiyo Mombasa kwa kuwa wazazi wake walikuwa wakiishi hapa na kwa sababu mazingira ya kijijini Mbitini hayakuwa rafiki kwa kazi yake ikizingatiwa kwamba watoto wengi katika maeneo ya vijijini hawavalii viatu.
Changamoto
Licha ya kuwa na uzoefu wa siku nyingi wa kushona viatu ilimchukua muda mrefu kupata mtaji wa kuanzisha kazi hiyo. Alipofika mjini Mombasa, anasema kuwa kazi hiyo aliianza na mtaji wa Sh425 na kwa sasa inampatia kipato kikubwa kinachokimu mahitaji yake ya kila siku.
Shida zingine anazopitia ni ukosefu wa malighafi ya kutengenezea viatu ikiwemo ngozi, vipini vya kufungia viatu ambavyo mara nyingi hukwamisha kazi yake na kukosa kutimiza ahadi anazowapatia wateja wake kupata viatu kwa wakati walioagana.
Alisema kuwa wateja wengine huweka oda na baadaye wakakosa kurudi hali anayosema kwamba huwa inampatia hasara kwa kuwa viatu hivyo vitakaa bila kupata mnunuzi.
“Mteja anapokuja kupima viatu na hatimaye asirudi huwa amekuweka katika njia panda usijue lipi la kufanya kwa kuwa viatu vile vitakaa bure pale na utakuwa huna pesa zingine za kununulia malighafi,”asema.
Wateja wake
Anasema kuwa kazi yake hunoga wakati wa shule zikifunguliwa kwa kuwa walengwa wakuu kwenye biashara yake ni wanafunzi, msimu wa shule huvuna donge nono kati ya Sh1,500 hadi Sh3,000 kwa siku.
Aliambia Akilimali kwamba biashara ikiwa chini huweza kupata kipato cha Sh45,000 na 90,000 kwa mwezi, amesema kuwa kazi hiyo imeweza kusomesha watoto wake katika shule ya upili na kujenga nyumba.
Anasema kuwa shule zinapofungwa huwa kazi yake inaenda chini sana kiasi kwamba mahitaji yake mengi hukwama kutokana na kukosekana wateja.
Aidha Daniel anatoa wito kwa vijana kuacha kuzembea mitaani na kutembea kwenye makampuni kutafuta ajira na wajitolee kufanya kazi ndogo ndogo za mkono akisema zitaweza kuwafungulia milango ya riziki.