Makala

BONGO LA BIASHARA: Vyombo vya ufinyanzi vilivyo sumaku kwa watalii

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na FRANCIS MUREITHI

TAKRIBANI kilomita 10 hivi kutoka mji wa Naivasha kuna karakana ambayo wakazi wengi wa mji huu hawana habari kuwa inaunda vyombo vya hali ya juu vya ufinyanzi.

Karakana hii ambayo inajulikana kama Fired Earth imeundwa chini ya miti inayotoa kivuli kwa wafanyakazi kutokana na miale ya jua kali na imejengwa kwenye shamba ambalo wakati mmoja lilimilikiwa na setla wakati wa enzi za mkoloni.

Hali ya utulivu, hewa safi na kelele za kuvutia za ndege kwenye miti na nyani wanaoruka kutoka mti mmoja hadi mwingine ndio kelele za kipeke ambazo utazisikia wakati unapotembelea karakana hii.

Kwa miaka mingi karakana hii ya ufinyanzi wa vyombo vya udongo imekuwa kivutio kikuu cha watalii wa ndani na wa mataifa ya ng’ambo ambao hupitia hapa kujinunulia bidhaa za ukumbusho wanapotembelea mji wa Naivasha.

Bidhaa zinazowavutia watalii ni pamoja na vikombe, sahani, mikebe ya udongo ya kupanda maua, vijiko, sufuria, nyungu na vikombe spesheli vya kunywa mvinyo.

Hali kadhalika unapotembelea karakana hii kwa mara ya kwanza waweza kujinunulia bidhaa kama vile vyombo vya kusimamisha mishuma kwenye meza ambavyo vimeundwa kwa mfano wa ndege maarufu wa flamingo miongoni mwa bidhaa nyingine nyingi.

“Nilianzisha karakana hii 2007 baada ya kufanya kazi ya kutengenza vyombo vya udongo na kuajiriwa na Larry Quton kutoka Marekani kwa kipindi cha miaka saba,” anasimulia Obadiah Kiragu ambaye ndiye mmiliki wa karakana hii.

Anaposimulia jinsi huchanganya udongo na kuufinyanga na kisha kuuchoma kwa moto mkali, Bw Kiragu humwacha mteja kinywa wazi kwa jinsi anavyoelewa kazi yake.

“Napenda sana kuchanganya udongo na kuuda vyombo vya udongo kwani kazi hii hunipa raha kila mara ninaunda vyombo ambavyo huwavutia watalii wa humu nchini na mataifa ya ng’ambo,” anasema Bw Kiragu.

Ili kuunda vyombo vya kuvutia, Bw Kiragu huchanganya udongo aina ya clay na maji ili kuufanya uwe mwororo na kisha huondoa vipande vya mawe na kuchanganya na kemikali aina ya kaoline.

Kisha awamu ya pili huwa kutoa vipande vya mawe yaliyosalia kwa kuzungusha udongo kwenye meza ya mbao kama mtu anayekanda unga wa kupika chapati.

Kisha baadaye udongo uliofinyangwa hutumbukizwa kwa mtambo unaozunguka ujulikanao kama kiln na kunyunyuziwa maji ili kuufanya uwe mwororo zaidi.

Baadaye huwekwa kwenye kivuli na kuanza kubadilika na kuwa rangi ya kijivu kabla kuanikwa kwa jua kwa siku mbili au tatu.

Bidhaa hizo kisha hupelekwa kwenye jiko la moto na kuchomwa kwa masaa kadha.

Baadaye mchoraji maalumu huweka michoro maridadi ya kisasa ya kuvutia kama vile maua, ndege, samaki, wadudu miongoni mwa michoro mingine inayo wafurahisha wanunuzi.

Hata hivyo, wateja wako huru kupendekeza michoro wanayotaka kwenye vyombo ambavyo wanatamani kununua.

“Rangi tunazotumia kuchora michoro kwenye vyombo vyetu haidhuru afya ya wateja wetu,” anasema Bw Kiragu.

Bw Kiragu anasema bidhaa zake huuzwa kwa bei nafuu kama njia mojawapo ya kuwavutia wateja wengi wanaotembelea mji wa Naivasha.

“Chombo cha kuweka sukari huzwa Sh1,800 ili hali vikombe na sahani huuzwa kwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000,” anasema Bw Kiragu.

“Wateja wangu wanaotamani kujifunza ufinyanzi ni pamoja na watoto, watu wazima na watalii. Mtu mzima mimi humtoza Sh1,500, watoto Sh1,000 na watalii Sh2,000 kwa mafunzo ya siku moja,” anasema Bw Kiragu.

Mafunzo yake yamekuwa kivutio kikubwa kwa baadhi ya wazazi wanaotaka watoto wao watimize ndoto zao za kuwa wasanii wa siku za usoni na watu wazima ambao hupendezwa na uchoraji.

Aidha anatoa mwito kwa wazazi ambao wamegundua watoto wao wana vipawa vya uchoraji kuwaleta kwenye karakana yake ili wapate mafunzo zaidi.

“Watoto wachanga walio na talanta za uchoraji hawapaswi kutumia muda wao mwingi wakicheza michezo ya video au kuona runinga kwani wakianza mafunzo mapema watapata kupanua mawazo yao ya uchoraji na sanaa,” anasema Bw Kiragu.

Na je kazi ii ya ufinyanzi inamletea faida?

“Licha ya hali ngumu ya uchumi, mimi sina la kujutia kwa kufanya kazi hii. Biashara ikinoga naweza kupata hata Sh50,000 kwa mwezi.”