BONGO LA BIASHARA: Wengi hawakuelewa kazi yake, lakini hakufa moyo
Na SAMUEL BAYA
NI bayana kuwa ubunifu na akili ya kutaka kufanikiwa inapomuingia mtu, kila fursa huiona kama inayomuelekeza katika kufanikisha hilo.
Hiyo ndiyo taswira kamili ya Bw Kelly Banda, mtaalamu wa masuala ya mauzo na mahusiano mema ambaye baada ya kukosa ajira katika sekta hiyo, alianzisha biashara ya kuonyesha fasheni na ulimbwende.
Huo ulikuwa ni mwaka wa 2011 mjini Kilifi na miaka minane baadaye hajutii kwa hatua aliyochukua.
Mradi wake wa Epitome Models umekuwa mojawapo ya miradi ambayo inaendelea kukua na kuimarika kila kunapokucha.
Katika mahojiano na ukumbi wa Akilimali, Bw Banda alisema alipoanzisha mradi wake mjini Kilifi, biashara hiyo ilionekana kuwa geni na wengi hawakufahamu kilichokuwa moyoni mwake.
“Wakati huo, hakuna mengi ambayo yalikuwa yakifahamika katika upande wa fasheni na ulimbwende, ila kwangu niliamini kwamba hii ni sekta ambayo nitaimudu na inaweza kunifikisha mbali,” akasema Bw Banda mwenye umri wa miaka 33.
Katika mahojiano yetu, Bw Banda alitueleza changamoto za ustawi wa biashara hii ambayo alisema ilikuwa vigumu kwake kuinawirisha katika eneo ambako haikuwa na mashabiki na wateja.
“Kwa kifupi, biashara hii inahusu kufundisha wasichana wanaotaka kuingia katika masuala ya ulimbwende na kuwapatia mbinu mwafaka wanazopaswa kufanya kuingia katika uanamitindo (modelling). Kisha baadaye tunawatafutia kandarasi katika kampuni au watu binafsi ambao wanataka kuwatumia kutangaza biashara zao,” akasema Bw Banda.
Alisema mbali na hilo, wao huamua kuwachukua walimbwende ambao wanataka kuingia katika shughuli hiyo ila hawana mahali pa kuanzia.
Licha ya kuanza akiwa chini na baada ya miaka miwili ya kuhangaika, alipata kazi ya kwanza mwaka wa 2013 wakati alipoandaa warembo katika kongamano la Miss Tourism Kilifi mwaka wa 2013/2014.
“Mimi ndiye niliyewatayarisha warembo ambao walishiriki katika mashindano hayo mjini Malindi. Baada ya hapo nilifanya matangazo kadhaa katika maeneo ya Watamu na Malindi ambapo niliwatayarisha warembo na waonyeshaji fasheni katika hafla mbalimbali na hapo ndipo sasa watu walianza kuifahamu biashara hii yangu,” akasema Bw Banda.
Kuandaa mashindano ya urembo
Yeye ndiye alikuwa muandaaji mkuu wa mashindano ya mrembo wa Kilifi mjini wa mwaka wa 2014/2015.
Ni mwaka huo huo ambapo pia alitayarisha mrembo wa Mazingira katika kaunti hiyo.
Aliyetawazwa mshindi katika nafasi hiyo ni Bi Josephine Tuva ambaye alikuwa ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Pwani kilichoko mjini Kilifi.
“Mashindano ya mlimbwende wa Mazingira yalifana sana na kwa mara ya kwanza yaliwafanya wakazi wa Kilifi, kuanza kushabikia sekta hii ya fasheni na ulimbwende. Nilitumia fursa hiyo kujiimarisha na sijawahi kurudi nyuma hadi wa leo,” akasema Bw Banda.
Mwaka wa 2016, walimbwende kutoka kwa shirika lake walishiriki katika ufunguzi wa hoteli moja eneo la Watamu katika biashara ambayo alipata Sh38,000.
“Nakumbuka kwamba hoteli hiyo ilikuwa inafungua biashara yake kwa umma na ilihitaji walimbwende kuwakaribisha wageni. Nilipata kandarasi hiyo ya usiku mmoja na kulipwa Sh38,000. Nilifurahi sana kwa fedha hizo,” akasema Bw Banda.
Mjasiriamali huyu ambaye yuko na Diploma ya mahusiano mema kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki pamoja na Digrii ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Kampala alisema kwa sasa yuko na walimbwende 18 katika taasisi yake, wote wakifanya kazi katika vitengo tofauti tofauti.
“Kwa kawaida na wakati biashara inapokuwa nzuri, mimi hupata Sh100,000 na mara nyingi huwa ni wakati wa likizo hasa mwezi wa Disemba.
Katika mahojiano yetu, Bw Banda alisema kuwa tayari wanafanya mpango wa kuvumisha vazi la ‘Kishutu’, ambalo ni nguo ya kiasili inayoendelea kupata umaarufu katika eneo la Pwani.
“Lengo langu kuu ni kuanzisha hafla ambayo itakuwa ikijulikana kama ‘Kishutu’ ili kuvumisha nguo hii ya asili ambayo inaendelea kupata umaarufu katika kizazi cha kisasa,” akasema Bw Banda.
“Tunataka hafla hiyo iwe inafanyika kila mwaka ili kuhamasisha kizazi cha sasa dhidi ya umuhimu wa nguo hiyo ya kiasili,” akasema Bw Banda.
Mbali na kuandaa hafla za fasheni na ulimbwende, Bw Banda na kikosi chake pia wamekuwa wakishiriki katika sekta ya upigaji picha za kitaalam, maarufu kama ‘professional photo-shoot’.
Katika mradi huo, jamaa huyu huzunguka katika maeneo mbalimbali ya Pwani ikiwemo katika fuo za bahari ambapo hupiga picha na kuweka katika mtandao wake wa kijamii.