BORA UHAI: Maana kamili ya msimu
Na EVANS MBUGUA
“Bora Uhai,” umekuwa msimu ambao umeteka mawimbi ya mitandaoni nchini Kenya kwa kishindo kikubwa. Mkenya amekuwa mtu ambaye hachagui maisha aishiyo kutokana na kadhia zinazomsonga kila siku.
Lake limesalia kutamani kuishi tu lakini si kuishi kwa hadhi maana wale anaowategemea kulainisha njia zake za kufurahia maisha ndio hao wanaomkandamiza.
Laiti wenye kumiliki nyenzo za kuzalisha mali wangemjali yuyu huyu Mkenya alowapa nafasi ya umilisi huo, Mkenya mwenyewe angekuwa akisema Uhai Bora bali si Bora Uhai.
Maana ni kuwa Bora Uhai na Uhai Bora japo yanaonekana kushahibiana maana/fadhiwa ni tofauti kabisa.
Mwafulani anaposema “Bora Uhai” ni ishara ya masikitiko,uchovu na mahangaiko tele. Huyo ni mtu ambaye amekata au anakatishwa tamaa na yule aliyemtarajia angemshujaisha.
Walakini, Mkenya atasemaje Uhai Bora badala ya anayosema sasa,’Bora Uhai,’ na hali inavyomwia ngumu!
Bora Uhai ni kauli nzuri ya kuelezea maonevu aliyonyooshewa Mkenya.
Mkenya ametamaushwa na ufisadi usokwisha,ufisadi ambao chanzo chake kipo lakini mwisho wake huonekani, wanaostahili kumkinga dhidi ya uonevu huu wanamwibia kila chake na hata uhai wanatishia kumpoka na ndipo hana budi kusema Bora Uhai.
Kabla ya kila uchaguzi ahadi huwa kemkem ambazo eti zitainuwa hali ya maisha ya Mkenya lakini wapi? Ona baada ya uchaguzi uliopita(2017) yale ambayo Mkenya ameletewa mashinani kama si siasa za mwaka wa 2022.
Wale ambao Mkenya aliwachagua ili watetee na kuimarisha hali yake sasa ndio hao wanatangatanga hata matangani wakijishaua vile wamejipanga kushinda uchaguzi wa mwaka 2022. Ni kweli kuwa kauli Uhai Bora haikuwa pata upenyu kwenye kamusi za wakenya wala kukita kambi kwenye kumbukizi zao.
Chakula kilichoko sokoni si salama tena. Kiungo muhimu katika chai-sukari,kimetiwa dosari. Nasema dosari maana madini ya Zebaki, Lead na Copper yanasemekana yametiwa. Wameamua kumwangamiza mwajiri wao mapema na ndipo mwajiri anaimba ‘Bora Uhai’.
Mkenya amekuwa akilipia huduma hewa,kodi hutozwa lakini faida yake haipo. Kodi zenyewe hupandishwa kila uchao huku hudumu zikidororeshwa makusudi na zingine kuondolewa daima na ndipo hadi leo magonjwa kama vile kipindupindu na utapiamlo yamesalia sugu.
Imekuwa mazoea uhai kunadiwa shilingi hamsini,maelfu wameangia barabarani kisa na maana kuna mlinda haki mahali fulani alichukua shilingi hamsini ili abiria wasafirishwe na dereva mlevi,dereva kisirani au waendeshewe gari kweche.
Masomo anayopata Mkenya hayamfaidi kitu,wangapi wamefuzu hata kwa uzamili na uzamifu na bado ni ombaomba? Usishangae hata viongozi wenyewe hawaamini elimu wanayodai kufadhili na kuifanya bure kwa yeyote yule lakini wapi,wameifanya bure isimfaidi yeyote.
Watoto wao husoma yale ya ughaibuni ambayo wanatumai yatawafaidi. Mazingira salama ya kuanzisha kazi na kujiendeleza kimaisha kwa kijana Mkenya hayapo, na ndipo usemi, ‘bora uhai’.
‘Bora Uhai,’ ni kauli inayoelezea hali anayoishi raia wa Kenya, ni dhihirisho hali si hali humu. Hali inavyoendelea kuwa hafifu naamini mkenya anajipurukusha ili kuinasua roho yake kutokana na mauti yasiyomwafiki.
Sijui atatumia mbinu ipi kuiokoa roho yake lakini njia zipo za kujisalimisha na ni muda tu hali ibadilishwe hata kama ni kwa ncha ya upanga maana hapo ndipo amani inaonekana kutuama: Tajiri dhidi ya Walalahoi.