Makala

Brenda Ogembo, malkia mpya wa raga ya Kenya

April 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA GEOFFREY ANENE

LICHA ya umri wake mdogo, Brenda Nyabiage Ogembo tayari ameanza kujizolea sifa katika raga ya Kenya.

Ogembo, 18, alifanya mtihani wa kidato cha nne katika Shule Upili ya Wasichana ya Eregi katika kaunti ya Kakamega mwaka 2023.

Aliibuka mfungaji bora wa miguso katika Ligi Kuu ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya msimu 2024 mnamo Aprili 6 akichezea Mwamba RFC.

Ligi hiyo ilijumuisha Mwamba, Northern Suburbs, Impala na Nakuru (Zoni ya Nairobi) na Shamberere, Rongo, Maseno na Western Spears (Zoni ya Magharibi).

Timu mbili za kwanza kutoka zoni hizo zilikutana katika nusu-fainali ambapo Mwamba walilipua Shamberere 81-0 ugani RFUEA jijini Nairobi.

Nao Northern Suburbs wakalemea Rongo 29-9 uwanjani Equip mjini Kitale.

Mwamba walikung’uta Suburbs 53-0 katika fainali ugani RFUEA.

“Nilianza kucheza raga katika muhula wa kwanza wa kidato cha tatu. Nilikuwa kiungo katika soka, lakini nikafifishwa matumaini na kocha,” alitanguliza Ogembo ambaye mashambani ni Kaunti ya Kisii.

Mtoto huyo wa pili na wa kike pekee katika familia ya watoto watatu, anasema alivutiwa katika raga na mchezaji wa kimataifa Janet “Shebesh” Okello aliyejiunga na MIE Pearls nchini Japan akitokea Mwamba mwaka 2022.

“Nilipata kuona video za Shebesh akichezea timu ya taifa ya Kenya Lionesses na kuvutiwa na uchezaji wake. Yeye ndiye shujaa wangu. Nilipenda utimkaji wake pamoja na anavyolinda mwili wake kama mwanaraga na pia si mtu mwenye maringo licha ya kuwa ana pesa,” akasema Ogembo.

Mwanaraga huyo anafahamika kwa majina ya utani ya Pogba na Dada Pogie aliyobandikwa na Claudia Muhavi akiwa Eregi na naibu wa nahodha wa Kenya Lionesses Judith Okumu, mtawalia.

Aliyapata kutokana na spidi yake kama mwanasoka wa Ufaransa, Paul Pogba.

“Ndugu zangu ni mashabiki wakuu wa raga licha ya kuwa ni wanasoka. Nimepata ujuzi kutoka kwao ambao ni muhimu katika raga kama chenga na kupiga mpira kufunga mkwaju. Mimi pia huenda nao mazoezi ya kukimbia kila asubuhi,” akaeleza kuhusu mchango wa familia yake katika safari yake.

Anasema mama yake amekuwa akimlipia nauli, kununua daluga na mavazi ya raga.

Ogembo, ambaye amelelewa na mama pekee tangu awe katika darasa la pili baada ya baba yake kufariki, alikuwa katika kikosi cha chipukizi katika ya umri wa miaka 14 na 18 walioshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Trinidad & Tobago mwezi Agosti 2023.

“Ndoto yangu kubwa ni kucheza raga ya malipo nchini Australia ama Canada,” akahitimisha.