Bridi mpya ya ng’ombe wa maziwa
SEKTA ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini imepigwa jeki kufuatia kuzinduliwa kwa kiinitete (embryo) kipya cha bridi ya ng’ombe aliyeboreshwa kutoka Brazil.
Bridi hiyo ya ng’ombe inajulikana kama Girolando, na imekuwa Kenya kwa miaka michache.
Hatua ya sekta ya ng’ombe wa maziwa kupigwa jeki, inatokana na kuletwa nchini kwa viinitete 350 vya Girolando kupitia Makongi Agri Limited na kampuni dada, Indicus Genetics, kwa ushirikiano na Ubalozi wa Brazil nchini Kenya.
Makongi Farm, kampuni ya ufugaji ng’ombe Eldoret, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Samvet Embriões, kampuni ya Brazil inayotoa huduma za ng’ombe.
Aidha, Makongi, inajishirikisha na huduma za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na wale wa nyama, ikiwa na lengo la kuboresha bridi.

“Tumekuwa tukifanya utafiti wa teknolojia ya embryo kuanzia 2015. Ziara ya kwanza Brazil ilikuwa 2010, na tunafurahia ushirikiano wa Brazil na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Idara ya Vetinari Kenya (DVS), na Kituo cha Raslimali za Jenetiki Nchini, sasa tumepata mwanya kuimarisha sekta ya mifugo,” akasema Tim Chesire Mkurugenzi wa Makongi Farm Director, Tim Chesire, majuzi wakati wa uzinduri wa kiinitete hicho kipya cha Girolando.
Girolando ni bridi ya ng’ombe wa maziwa anayefugwa Brazil, na anayesifiwa kustahimili mikumbo ya mabadiliko ya tabianchi kama vile kiangazi, ukame na hali ya hewa.
Spishi hiyo haina changamoto na malisho, na inakadiriwa kuzalisha wastani wa lita 17 za maziwa kwa siku kwa kushabikia nyasi za kawaida.
“Girolando haihitaji nyasi kama vile silage au chakula cha madukani ili kuzalisha kiwango hicho cha maziwa. Inahimili mikumbo ya tabianchi,” akaelezea Chesire.
Kiinitete – embryo ni steji ya kwanza ya ukuaji wa ndama, ambayo huundwa na shahawa – manii (sperms) zinapotungisha yai ujauzito kwenye ng’ombe.
Hutumika kujamiisha, na kuwezesha wakulima kupata bridi bora ya mifugo wenye jenetiki zenye nguvu.

Aidha, embryo hugandishwa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye.
Kando na viinitete 350 vilivyoletwa nchini, Mkurugenzi wa Makongi Farm, alifichua kwamba kampuni yake kwa ushirikiano na Kituo cha Raslimali za Jenetiki Nchini na serikali, ina mpango kuongezea viinitete vingine 1,500.
Vitasambazwa katika kaunti mbalimbali kusaidia wakulima kupata bridi mpya ya Girolando, na pia nchi zingine Barani Afrika.
Balozi wa Brazili nchini Kenya, Silvio Albuquerque, kwenye mahojiano alisema kuzinduliwa kwa embryo za ng’ombe aina ya Girolando ni hatua kubwa kuboresha sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa hapa nchini.
“Italeta mabadiliko katika uzalishaji wa maziwa, kuongeza kiwango na pia kuwa na ng’ombe wanaostahimili athari hasi. Girolando, ni ng’ombe ambaye jenetiki zake zimeimarishwa na sehemu anazofugiwa Brazil si tofauti na za Kenya,” akasema Balozi Silvio.
Alihimiza Kenya kukumbatia utaalamu wa Brazil hasa katika teknolojia ya ufugaji, ili kuangazia suala la usalama wa chakula.
Uzinduzi wowote ule wa bridi mpya ya mifugo Kenya sharti uidhinishwe na Idara ya Vetinari na Kituo cha Raslimali za Jenetiki Nchini.

Asasi hizo mbili za serikali zilisaidia kuhakikisha embryos za Girolando zimefuata taratibu zilizowekwa.
Kulingana na David Ojigo, Naibu Mkurugenzi Idara ya Vetinari, jenetiki au bridi yoyote ile ya mifugo lazima iafikie vigezo vya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), sheria za Ushirika wa Kimataifa wa Uhamishaji wa Kiinitete na DVS.
Kenya, ng’ombe aina ya Girolando anauzwa Dola za Amerika 3,000 (Ksh390, 000), na Brazil anagharimu Dola 1,200 (Ksh155, 000).
Kuboresha sekta ya ufugaji nchini, wakulima wamekuwa wakitegemea teknolojia ya uhamilishaji (AI) ambayo ukumbatiaji wake unaendelea kushuka.
Sekta ya ufugaji inachangia asilimia 12 ya ukuaji uchumi (GDP) kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja.
Kulingana na data za Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Kenya ina karibu ng’ombe 5.1 wa maziwa, na mwaka 2023 taifa lilizalisha lita bilioni 5.2 za maziwa – kiwango kinachokadiriwa kuwa cha thamani ya Sh312.7 bilioni.