Makala

BURUDANI: Hizi hapa sababu za baadhi ya watu kupenda kusikiliza muziki

October 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

KAMA unapenda kusikiliza muziki basi bila shaka una sababu mbalimbali.

Muziki hutufanya tuwe na furaha

Kusikiliza muziki huzalisha kemikali ya dopamane ambayo hutufanya tujisikie vizuri. Hii ndiyo sababu mtu akiwa anajisikia vibaya au kukosa furaha mara nyingi anaposikiliza muziki hasa wa taratibu, hujisikia vizuri.

Hivyo basi, wakati ukiwa umekosa raha unaweza kusikiliza nyimbo unazozipenda.

Muziki huondoa msongo wa mawazo na kuboresha afya

Kusikiliza muziki hupunguza kwa asilimia kubwa homoni zinazosababisha msongo wa mawazo. Ikiwa basi msongo utapungua ni dhahiri kuwa pia maradhi mengi ambayo chanzo chake ni hiyo hali ya kusononeka, yatapungua kama si kuisha kabisa. Unaweza kusikiliza muziki na kuimba wakati muziki unapoimba; pia usisahau kucheza angalau kwa kuchezesha miguu ili kupata ‘tiba’ hii kamili.

Hukuwezesha kulala vizuri

Kusikiliza muziki husafisha ubongo wako na kuuweka katika hali nzuri itakayokuwezesha kupata usingizi mzuri.

Ni dhahiri kuwa mziki una nafasi kubwa katika kulala kwetu. Inashauriwa wakati wa usiku kuweka ubongo wako katika hali nzuri ili uweze kulala vyema; unaweza kusikiliza mziki wa taratibu kabla ya kulala.

Hukuwezesha kujifunza na kukumbuka

Baadhi ya watu wamebainisha kuwa wanaposoma au kujifunza mambo kadhaa wakati wakisikiliza muziki, basi hufanikiwa kuyamudu maswala hayo vyema.

Hukukumbusha mambo

Ni dhahiri kuwa nyimbo nyingi huambatana na matukio au vipindi fulani vya muda kwa maana kuwa husheheni.

Si jambo la kustaajabisha ukasikia muziki fulani ukakukumbusha matukio au eneo fulani ulilokuwa zamani. Watu wamekuwa wakikumbushwa matukio ya furaha kama vile ndoa, mahafali, au hata ya uzuni kama vile misiba na maradhi. Hivyo ni wazi kuwa kwa njia ya mziki tunaweza kukumbuka matukio au watu fulani tuliowahi kukutana nao maishani mwetu.