Makala

BURUDANI: Lucy Blessed asema lengo ni kufikia upeo wa juu

November 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER CHANGTOEK

NI msanii wa nyimbo za Injili ambaye anachapukia tasnia hino ya uimbaji.

Japo jina lake huenda halijajulikana ghaya ya kujulikana kwa waja wengi, amejifunga kibwebwe kusudi ahakikishe kwamba anapiga hatua katika sanaa na hata kufikia upeo wa juu katika siku za usoni.

Ni msanii Lucy Njeri, ambaye anajulikana kwa jina la usanii kama Lucy Blessed.

Anatarajia kuyaona makubwa kwa uga wa usanii katika siku za halafu. Fauka ya hayo, anaazimia kushirikiana na wasanii wenye majina makubwa katika katika siku za usoni.

“Mimi ni Lucy Njeri, na ninajulikana kwa jina langu la usanii kama Lucy Blessed,” ajitambulisha msanii huyo, akiongeza kuwa alianza uimbaji Aprili 2016.

Msanii yuyo huyo, anafichua kuwa aligundua kuwa alikuwa na kipaji cha kuimba miaka mitano iliyopita.

Msanii Lucy Njeri, ambaye anajulikana kwa jina la usanii kama Lucy Blessed. Picha/ Peter Changtoek

Hata hivyo, alianza kuutunga wimbo wake wa kwanza mnamo Aprili 2016, na wimbo huo unajulikana kwa jina Mahoya.

Kufikia sasa, msanii huyo amefanikiwa kuzirekodi albamu tatu, ambapo albamu yake ya kwanza inajulikana kama Mahoya.

“Niliirekodi albumu yangu ya kwanza, Mahoya, katika Taji Studio, Kitengela na hizi nyingine mbili; Kirathimo na Ciumbuka, nikazirekodi katika studio inayojulikana kama Quality Media, Ruaka. Niliamua kuziimba za Injili kwa sababu ni wito kutoka kwa Mungu,” asema Njeri.

Anafichua kuwa alichochewa na mwimbaji mmoja anayeitwa Obedee Obed, na akaamua kuziimba nyimbo zizo hizo.

Anasema kwamba alizitumia hela nyingi kuirekodi albamu moja. “Pesa zinazohitajika kuirekodi albamu moja ni kuanzia Sh50,000 hadi Sh60,000.”

Kama zilivyo tasnia nyinginezo, kuna baadhi ya changamoto ambazo amewahi kuzipitia. “Kutoa sidii nyingi lakini zote huwa hazinunuliwi. Wengine hulalamika kuhusu bei ninayouza sidii zangu. Kughushiwa kwa sidii pia ni changamoto nyingine,” afichua msanii huyo.

Anasema kwamba sidii zake hupatikana jijini Nairobi, kwa maduka ya kuuza santuri za muziki, na aghalabu katika eneo la Nyamakima.

“Hata mtu anaweza kupiga simu ili nimletee katika pahali aliko, kama yeye ni mteja,” asema Njeri, akiongeza kwamba amezirekodi video za nyimbo zake.

Wimbo wake uliovuma sana unajulikana kwa jina Ciumbuke.

Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika shughuli ya uimbaji wa nyimbo za injili wangoje wakati waliopangiwa na Mungu.

Japo msanii huyo hajabainishi bayana kiasi cha hela anazozipata kwa shughuli ya utungaji na uimbaji, anasisitiza kuwa muziki unalipa vyema.

“Katika siku zijazo, ninapanga kutoa nyimbo nyingi na pia kurekodi muziki kwa kushirikiana na wasanii wanaotambulika kama vile Ringtone, Shiro wa GP na Chege wa Willy,” adokeza Njeri.