Makala

BURUDANI: Madam Vicky wa kipindi cha 'Maria' ataka serikali itie zingatio katika kuinua sekta ya uigizaji nchini

December 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI mwanamitindo wa muda mrefu na miongoni mwa wanamaigizo wanaovumisha kipindi cha ‘Maria’ ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV ambapo huzalishwa na Jiffy Pictures.

Anasema alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo bila kutarajia lakini ni talanta anayopania kuikuza zaidi. Sheila Ndanu ambaye kwa jina la msimbo (usanii) anafahamika kama Madam Vicky ameibuka kati ya vivutio vya wengi katika kipindi hicho kilichoanzishwa mwaka uliyopita.

”Ingawa nilikuwa napenda kutazama kipindi cha Mali, binafsi sikuwahi fikiria kama ipo siku nitashiriki masuala ya burudani ya uigizaji. Lakini mwaka jana ndio nilisukumwa nianze kushiriki katika kipindi hicho kama mamake Vicky,” anasema na kuongeza kuwa alianza kama mzaha lakini uigizaji umeibuka ajira kwake.

Anasema anajihisi mwenye furaha tena sana maana amebahatika kuibuka kati ya wasanii wanaoshiriki kipindi cha Maria kinachojivunia kujizolea wafuasi wengi tu ndani ya mwaka mmoja.

LYNN WHITFIELD

Katika mpango mzima anasema anatamani sana apate kazi zingine za uigizaji huku akipania kupalilia talanta yake kufikia kiwango cha kimataifa. Anadokeza kuwa ingawa ni mgeni kwenye gemu analenga kufikia hadhi ya mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Marekani aitwaye Lynn Whitfield aliyeshiriki filamu kwa jina Greenleaf. Anadokeza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo ana imani atakuwa anatosha mboga kushiriki filamu za kimataifa.

”Nimegundua kwamba wakati wa Mungu hakuna anayeweza kuuzuia maana sikutambua kama nina talanta ya uigizaji lakini hatimaye nimejipata katika jukwaa hilo,” akasema.

KAUNTI 47

Anatoa wito kwa serikali za Kaunti zote 47 kote nchini zianzishe vituo vya kutoa mafunzo kwa waigizaji wanaokuja ili kutambua vipaji vyao mapema. Pia anasema itakuwa vyema kama serikali inaweza kuwa inafadhili wasanii wanaoibukia ili kujiunga na vyuo husika kusomea masuala ya maigizo.

Kwa waigizaji wa humu nchini Madam Vicky anasema angependa sana kufanya kazi na wasanii kama Neomi Ng’ang’a na Mary Gacheri walioshiriki filamu kama Maempress na Mali mtawalia. Barani Afrika anawazia kupanda jukwaa moja na wanamaigizo wa filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Rita Dominic na Patience Ozokwor.

Sheila Ndanu anayefahamika kama Madam Vicky. Picha/John Kimwere

CHANGAMOTO

Madam Vicky, 55, anasema mwanzoni alipitia kipindi kigumu hasa kuelewa mistari yake kulingana na script.

”Ingawa nilikuwa zimezoea masuala ya wanamitindo nilipoanza uigizaji nilikuwa muoga sana. Lakini licha ya hayo tayari ninaendelea kuimarika kila uchao sina matatizo kama mwanzoni.” Anadokeza kuwa anajivunia kugundua ana talanta ya uigizaji ambapo amebahatika kutumia sehemu ya mapato yake kusaidia watoto mayatima pia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi.

Mwigizaji huyu anashukuru serikali kwa kuhidhinisha taifa hili kuwa na mfumo wa mashirika mengi ya habari kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita.

Hata hivyo imechangia wengi wakiwamo wanamaigizo kupata ajira kwenye vyombo vya habari nchini.

”Mfumo huo umechangia kuwepo ushindani mkubwa hali inayolenga kupaisha tasnia ya filamu nchini,” alisema na kuongeza kuwa waigizaji wa Kenya wanapiga hatua wanakolenga kufikia wenzio wa filamu za Hollywood.