BURUDANI: Mtunzi anayelenga kuwafaa wasanii chipukizi na wanaotia fora
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
KILA mwanafunzi anayesomea shule ya upili na chuoni, huwa anachagua masomo yatakayomfanya afanikiwe kwa kazi atakayoipenda kufanya baada ya kukamilisha kiwango fulani cha masomo yake.
Fatma Mohamed Ali alipokuwa mwanafunzi wa Mbaraki Girls alipendelea kuwa mtunzi wa mashairi na aliazimia atakapomaliza, awe miongoni mwa washairi watakaokuwa wakiwatungia nyimbo wasanii chipukizi na hata wale wenye majina makubwa walioko eneo la Pwani.
“Nilipenda sana kutunga mashairi na azma yangu kubwa ilikuwa ni kuwa mshairi wa kuwatungia nyimbo za mafunzo washairi wanaoinukia pamoja na wale ambao tayari wana majina makubwa kwani nitakuwa nami nimejitambulisha,” akasema Fatma.
Kwa wakati huu, msichana huyo anayesoma masomo ya kuwa mpokezi wa wageni katika ofisi za kampuni za wamiliki binafsi na mashirika makubwa ya kiserikali anasema angependelea kupata wasanii ambao watahitaji kutungiwa mashairi yakiwemo kazi kama nyimbo ili awafanyie kwa malipo.
“Kila kazi mtu unayofanya inahitaji malipo nami najiingiza fani hii ya utunzi wa mashairi ili ipate kunisaidia kupata pesa za kuendeleza kipaji changu pamoja na kujipangia maisha yangu ya baadaye,” akasema mtunzi huyo.
Kwake yeye anasema anapendelea kutunga nyimbo zenye maadili mema na mafunzo ya kuwaidhia watu wafuate mambo mema na pia kuwasihi vijana wainukie katika mazingara mazuri yasiyokuwa ya kuharibu majina ya familia zao.
“Nafikiri kwa ajili ya kuwa mtunzi wa nyimbo, niko kwenye fani ya muziki ambayo ni mojawapo ya mambo ambayo yananikosha na niyapendayo. Naamini wanamuziki wanahitaji watunzi wa kuwatungia nyimbo ambayo zitafuatana na mahadhi yao,” akasema Fatma.
Aliomba kufanyike mikakati ya baadhi ya washairi wenye kupenda muziki, kuunda chama chao ambacho kitakuwa na wanachama watakaoajiriwa na waimbaji wakihitaji mashairi.
“Ni muhimu kwa washairi nao wawe sehemu ya fani ya muziki,” akasema Fatma.
Mshairi huyo anasema ameamua kusomea masomo ya kuwa mpokezi wa wageni katika ofisi kwa ajili anatambua kuwa kuna umuhimu wa mtu kujua namna ya kupokea wageni hasa kwenye ofisi za kampuni na mashirika makubwa yanayotambulika kimataifa.
Mbali na kujihusisha na mashairi, Fatma kwa wakati huu anatafuta njia ya kuwa ‘model’ wa kupigwa picha na makampuni yatakayotaka kutangaza biashara zao. “Ninapendelea sana kujiunga na fani ya kupigwa picha za kutangaza biashara mbalimbali,” akasema.
Kwa upande wa muziki, Fatma anapendelea zaidi kusoma vitabu vya hadithi na kusikiliza muziki. “Napenda sana kusoma vitabu vya hadithi aina mbalimbali na kusikiliza nyimbo za mitindo ya Bongo Fleva na Hiphop,” akasema.
Fatma amesema wasanii wa eneo la Pwani wanahitajika kuimba nyimbo za mapenzi lakini zenye mashairi yenye kutoa mafunzo kwa wapendanao.
“Hakuna haja ya kuimba nyimbo zenye maneno ya kukosa adabu kwani tunawafanya watoto waige na hivyo si vizuri,” akasema.
Fatma aliwataka waimbaji wa Pwani wafanye mipango ya kusafiri na kuimba kwengineko nchini na nchi jirani za Tanzania na Uganda ili wapate kujionea jinsi wasanii wa sehemu hizo wanavyopata ushauri.
Aliwapongeza wasanii waliohamia jijini Nairobi kwa kuchukua hatua hiyo kwani hivi sasa wanaendelea kupiga hatua ya kuinua vipaji vyao. Alimtaja msanii msichana kutoka Mariakani, Boomer Best kama mmojawapo wa wasanii waliopiga hatua kubwa kutokana na kuhamia Nairobi,” akasema.
Fatma pia amewashauri viongozi wa Pwani wawasaidie wasanii wanaoinukia kwani sehemu nyingine za nchi pamoja na huko Tanzania ambako serikali inajihusisha zaidi kuwasaidia waimbaji wao.