Makala

Cha kufanya kupata pesa ambazo Meta imetangaza

March 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

ILI wapakiaji maudhui nchini Kenya wanaotumia mitandao ya Facebook na Instagram inayomilikiwa na Meta kuanza kulipwa kuanzia Juni 2024, watahitajika kutimiza masharti kadhaa.

Kulingana na kampuni ya Meta, ambayo inamiliki mitandao hiyo miwili, kuna masharti kadhaa ambayo wanakontenti hao watalazimika kutimiza ili kupata malipo hayo.

Masharti hayo yanaangazia akaunti ya Facebook au Instagram ya mwanakontenti husika na video atakazopachika katika akaunti yake.

Kwa video zitakazopeperushwa moja kwa moja au mbashara, lazima mtu awe na angaa wafuatiliaji  5,000 katika akaunti yake ya Instagram au Facebook. Lazima video  atakazokuwa  ameweka katika akaunti yake ziwe zimetazamwa kwa dakika  60,000 kwa muda wa siku 60 zilizopita. Kwa video zilizopeperushwa moja kwa moja, lazima ziwe zimetazamwa kwa angaa dakika 600,00 kwa muda wa siku 60.

Lazima ukurasa uwe na angaa video tano, zikiwemo video tatu zilizopeperushwa na mwenye akauti mwenyewe.

Masharti mengine ni kwamba lazima mwanakontenti awe amefikisha umri wa miaka 18, awe na video tano zinazotazamwa kwa wingi katika akaunti yake ya Facebook.

Ili kutimiza  mitazamo ya jumla ya dakika 60,000 katika siku 60 na ikizingatiwa kuwa mwanakontenti ana wafuatiliaji 5,000 hilo linamaanisha kwamba kila mfuatiliaji anafaa kutazama video kwa muda wa sekunde 30 kiwastani kila siku.

Kulingana na mwanakontenti Timothy Kimani, maarufu kama ‘Njugush’, hatua hiyo ni nzuri, kwani itawawezesha watu wengi wanaoweka video zao kwenye mitandao ya kijamii  kufaidika, japo anasema kuwa serikali haifai kuwakata kiwango cha juu cha ushuru.

“Watu wengi watakaofaidika kutokana na mwelekeo huo mpya ni vijana. Ikizingatiwa wengi wao hawana ajira, wito wangu kwa serikali ni kuhakikisha hata ikiwa watakatwa ushuru, si kwa kiwango ambacho kitawaumiza,” akasema Njugush, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mcheshi Brenda Gatwiri, anayefahamika kama ‘Gatwiri’ kwenye mitandao ya kijamii.