• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Chamwada azungumzia alivyojiuzulu Citizen TV akiwa hana ndururu

Chamwada azungumzia alivyojiuzulu Citizen TV akiwa hana ndururu

NA LABAAN SHABAAN 

Alex Chamwada kwa ufupi:

  • Alivyoanza Kampuni ya Chams Media Akiwa Msoto
  • Alijiuzulu Kuajiriwa na vyombo vya habari bila pesa na akiba
  • Alianza Chams Media akiwa na simu na laptop. Ilikuwaje?
  • Alichukua nyumba kwa mkopo na madeni yakazidi sana ikabidi auze ili alipe deni la nyumba hiyo
  • Alikuwa mwanahabari maarufu sana aliyetembea dunia lakini akajiuzulu akiwa hana pesa
  • Anasema ni Idea ya kuanzisha kampuni yake tu alikuwa nayo bila mtaji wowote

MWANAHABARI Mashuhuri Alex Chamwada, 53, alijiuzulu kazi ya utangazaji mwaka wa 2014 na kutafuta maisha kwa njia nyingine akiwa ‘msoto’ baada ya kufanya kazi ya utangazaji kwa takriban miaka 20.

Kufikia kipindi cha kuaga ajira, alinuia kuanza kazi yake binafsi ya kuandaa habari na makala maalum akiwa mtangazaji huru lakini kukosa akiba ya pesa, achia mbali hata kamera, kulikuwa changamoto kubwa.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo katika podkasti ya Dau la Maisha, Bw Chamwada alifunguka kuwa mamilioni ya pesa aliyovuna tangu miaka ya tisini kazini ziliishia kusomesha ndugu zake na kuganga kansa iliyomuua baba yake.

“Sikuwa na pesa baada ya kutoka chumba cha habari nikiwa na marundo ya madeni. Baba alituacha licha ya kutumia pesa zote kutibu kansa,” alitanguliza.

“Nilikuwa ‘ninang’ara’ kwenye TV lakini pesa ziliishia nyumbani kwa mikopo na kusaidia familia,” akaongeza.

Bw Chamwada alipekua buku lake la kumbukumbu na kuweka paruwanja jinsi ilibidi auze nyumba ambayo alikuwa analipia kwa mkopo (morgage): Ni nyumba aliyokusudia kufanya makazi yake ya kudumu.

Anaarifu kuwa kadri alivyong’ang’ana kumaliza mkopo ndipo upeo wa kukamilisha deni ulionekana mbali.

Ili kumaliza msongo uliomzonga wa kumaliza mkopo huo, Bw Chamwada hakuwa na budi ila kuuza nyumba apate fedha ya kumaliza deni.

Anasikitika kuwa ni kwa njia hiyo ndivyo alipoteza makazi na pesa zake – hata hivyo, alipata afua.

Bila Mtaji Alianza Vipi Chams Media Limited?

“Si lazima uwe na pesa mkononi ili uanze biashara. Nilianza kampuni yangu na laptop na simu. Sikuwa hata na nauli lakini wazo lilizaa pesa. Nilikuwa ninatembea miguu hadi Nation Centre kuleta sampuli ya vipindi vyangu,” Bw Chamwada anavuta taswira nyuma alivyoanza kampuni yake ya mawasiliano, Chams Media Limited, kutoka sufuri mwaka wa 2013.

Ulikuwa mwaka mmoja kabla ya kutoroka ajira sababu ya ukinaifu na kusaka changamoto mpya.

Shirika lake linajulikana kwa kipindi cha televisheni cha Daring Abroad ambacho hupeperushwa katika runinga ya NTV kila Jumamosi saa moja unusu.

“Nilipoanza niliandaa vipindi nikidhani vyombo vya habari vingenunua vipindi vyangu. Lakini kwa mwaka mmoja hakuna stesheni ilichukua vipindi vyangu,” Bw Chamwada alisikitika.

“Nilikuwa ninatembea miguu kuingia jijini kuja hapa Nation Centre ili nilete vipindi vyangu bila mafanikio,” akaongeza.

Aliunda msingi mzuri wa kufana alipoanza kutafuta wafadhili waliotaka kujinadi kwenye runinga.

Hapo ndipo aliona hakukumhitaji kuwa na fedha kuanzisha kazi yake.

Kuwa na tajiriba na umaarufu kulimsaidia kuvutia wafadhili walioamini uwezo aliokuwa nao.

“Wateja hunitafuta wakitaka makala yao yapeperushwe kwenye TV fulani na hulipia gharama ya utayarishaji na matangazo,” alisema.

Kutembea Kwingi Ndiko Kuona Mengi.

Alipokuwa mwanahabari wa vituo vya Habari vya Kenya Broadcasting Corporation (KBC), Royal Media Services (RMS), Standard Group (SG) na Voice of Amerika (VOA) kati ya mwaka wa 1994 na 2014, alifaulu kuzuru mataifa ya ughaibuni.

Bw Chamwada anaeleza alivyokutana na Wakenya waliokuwa wajasiri na kuvuka boda ili wapate mali.

“Kutembea kwingi duniani kulinikutanisha na Wakenya wakiwa nchi nyingine wakitega uchumi. Hapo ndipo wazo la Daring Abroad lilianzia,” anafichua.

Kupitia kipindi hiki, Bw Chamwada huangazia Waafrika wanaosaka tonge ndani na nje ya bara Afrika.

Kadhalika, ameendelea kumwaya mwanga wa kurunzi yake kwa wasio waafrika wanaofana barani.

Ujasiri Ulivyomwezesha Kutangaza Katika Idhaa ya Taifa KBC Akiwa Chipukizi

Akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Moi, Mwanzilishi wa Chams Media alifika jijini Nairobi kwa mara ya kwanza mwaka wa 1994.

Ni mwaka huo ndio alikutana na mtangazaji, James Mwaura, aliyependa kumsikiza sana redioni.

Na alipokutana naye, maisha yake yalibadilika na akaanza kuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi chuoni na kwao kijijini.

“Kuna watu wana roho nzuri. Bw Mwaura alinikaribisha KBC na akapima sauti yangu iliyokuwa na athari ya lugha ya mama (Kimaragoli) ila alisifia Kiswahili kizuri kisha akanifunza jinsi ya kuandika,” alikumbuka.

“Nilipotuma habari mara ya kwanza, Bw Mwaura aliipeperusha hewani,” alikumbuka kwa furaha.

Kwa sababu ya ukarimu huu, ndiyo Bw Chamwada alianza kujulikana na hatimaye akapewa nafasi ya kutangaza katika vipindi vya watoto redioni KBC.

 Mcheza Kwao Hutuzwa na Kutunzwa.

Juhudi zake za kutangaza habari za kuhamasisha jamii zilimfanya akatambuliwa na marehemu Rais Mwai Kibaki.

“Mwaka wa 2010 ofisi ya Rais iliniita ikasema imenitambua kwa huduma bora (Order of Grand Warrior (OGW)) sababu ya kuripoti habari za kuelimisha umma,” alisema.

Kisha akarejelea tuzo nyingine, “Mwaka wa 2022 nilipata MBS baada ya kutambuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta nikiwa mwanahabari huru kwa kuendesha Chams Media. Ilinisaidia kwa kuwa kila ninakoenda huwa ninatambulika.”

Vile vile Bw Chamwada anakumbuka alivyofadhiliwa kusoma masuala ya kilimo na utoshelevu wa chakula katika Chuo Kikuu cha Oklahoma State mwaka wa 2011 kwa kuwa mtangazaji mahiri aliyeangazia masuala ya kilimo.

“Wengi walianza kunijua nilipokuwa ninaripoti kutoka Amerika jijini Washintong DC kuhusu uchaguzi mkuu wa Amerika,” aliarifu.

“Baadaye nikaripoti kutoka Hague Uholanzi bado nikiwa mtangazaji wa Runinga ya Citizen,” akaongeza.

Malezi na Masomo

Aghalabu yeye hujiita kijana wa kijijini aliyefaulu kuselelea na kufaulu jijini.

Bw Chamwada alizaliwa mnamo Agosti 16, 1971 kijijini Elongo, eneobunge la Sabatia, Kaunti ya Vihiga.

Ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto 12 na aliishia kutegemewa kuwasomesha na kuwatunza wazazi wake.

“Wazazi waliuza ng’ombe ili wanisomeshe na sasa nimefaulu kuwarejeshea ng’ombe na mama anafurahi ninavyowatunza,” akasema.

Alisoma katika shule ya msingi ya Elongo, Vihiga na shule ya upili ya St Peters Mumias, Kaunti ya Kakamega.

“Nilisoma masuala ya Sayansi ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Moi na kufuzu 1996,” aliweka wazi akidhani ilikuwa kozi ya uanahabari.

“Nilidhani ni kozi ya utangazaji. Nilienda huko nikashangaa. Watu walinitania kuwa ninasomea mambo ya kupanga vitabu. Katibu wa Msimamizi wa Masuala ya Wanafunzi Chuoni (Dean of Students) karibu anipige kofi nilipoenda kubadili kozi ili kusomea uanahabari,” alikumbuka akitabasamu.

Baadaye alisoma Diploma ya Juu katika Masuala ya Uanahabari katika Chuo Kikuu cha Nairobi kabla ya kupata shahada ya uzamili kuhusu Siasa na Vyombo vya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza.

  • Tags

You can share this post!

Mchezo wa kisiasa aliocheza Riggy G uliomfanya Ndindi Nyoro...

Kando na Eliud Kipchoge, wafahamu ‘macelebs’...

T L