CHANGAMOTO: Chanzo cha vifo vya uzazi na jinsi ya kudhibiti hali
Na MARY WANGARI
MIONGONI mwa hatua zote za ukuaji katika maisha ya mwanadamu, bila shaka ujauzito ndilo tukio la kustaajabisha zaidi.
Kuwa na kiumbe anayekua ndani ya mwili wa mama kwa miezi tisa ni jambo ambalo maneno pekee hayatoshi kusawiri taswira kamili.
Huwapa wanawake fursa ya kuwa waumbaji washiriki pamoja na Maulana.
Hata hivyo, si wanawake wote walio na bahati ya kufurahia tukio hili. Kwa baadhi ya wanawake, ujauzito huambatana na madhila chungu nzima na hata kifo.
Ripoti mpya iliyochapishwa na Shirika la Afya Duniani-WHO mnamo Machi mwaka huu, inadhihirisha kwamba wanawake 830 hufariki kila uchao kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.
Nchini Kenya, kwa kila visa 100,000 kina mama 362 hufariki huku idadi ya watoto wachanga wanaofariki ikiwa 22 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya BMC kuhusu Athari ya Sera ya Huduma ya Afya ya Uzazi bila Malipo.
Sababu zinazochangia vifo
• Maambukizi baada ya kujifungua
• Shinikizo la damu kwa kina mama
• Kuvuja damu kupita kiasi wakati wa kujifungua
• Uchungu uliokithiri (Prolonged labour)
• Matatizo yanayotokana na uavyaji mimba.
Hali hii inaweza kudhibitiwa na kuokoa maisha ya wanawake na watoto wachanga endapo kina mama watapokea huduma ya afya kutoka kwa matabibu wenye ujuzi kabla ya ujauzito, wakati wa kipindi cha kubeba mimba na hatimaye baada ya kujifungua.
Ni sharti kuwepo mikakati madhubuti na ushirikiano mwafaka baina ya wadau ili kudhibiti hali hii na kufanikisha Malengo ya Ustawishaji Maendeleo 2016 – 2030 ambapo dhamira mojawapo ni kupunguza vifo vya uzazi hadi chini ya 70 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa.
Licha ya kuongezeka kwa vituo vya afya nchini, imeripotiwa ni asilimia 61.2 pekee ya kina mama wanaojifungua katika vituo vya afya.
Utafiti unaonyesha kuwa licha ya idadi kubwa ya wanawake nchini kuhudhuria kliniki kabla ya kujifungua, ni wachache mno wanaoenda kujifungua katika vituo vya afya.
Wengi wao huamua kujifungua manyumbani wakiwa pekee yao, kupitia usaidizi wa wanawake wenzao au kupitia usaidizi wa wakunga wa kienyeji.
Kiini kikuu cha vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi kinachangiwa pakubwa na kina mama kujifungua bila wahudumu wenye ujuzi.
Ili kudhibiti hali hii, Kenya ilijiunga na mataifa mengine ya bara Afrika kufutilia mbali ada ya huduma za uzazi iliyokuwa ikitozwa katika vituo vya umma. Sera mpya inasimamia aina yote ya kujifungua ama kupitia njia ya kawaida au upasuaji.
Japo kuondoa ada ya kujifungua ni mwafaka, kuchelewa kuamua kuhusu huduma za uzazi kutoka kwa wahudumu wa afya, kuchelewa kufika katika vituo vya afya, na kuchelewa kupokea matibabu ya kutosha au kupata rufaa haraka ni tatizo kubwa.
Hofu ya kudhulumiwa na maafisa wa afya, kukosa uhamasishaji, ufukara, itikadi potovu za kitamaduni, ni baadhi ya sababu zinazotajwa na Dkt Isaack Bashir ambaye ni kinara wa Mradi wa Kuwezesha Kuongezeka kwa Upangaji Uzazi Mashinani (DIFPARK) katika Futures Group, na ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi katika Wizara ya Afya.
Masuala mengineyo ya kiuchumi, ukosefu wa usawa katika mifumo ya afya, kiwango cha ubora wa huduma za uzazi katika vituo vya afya pamoja na masuala ya kisiasa, kijamii, kimazingira na kidini ambayo huenda yakaathiri matumizi na matokeo ya huduma ya afya ya uzazi nchini Kenya bado hayajatiliwa maanani.